Home BUSINESS KIWANDA CHA SUKARI MKULAZI KUANZA UZALISHAJI HIVI KARIBUNI

KIWANDA CHA SUKARI MKULAZI KUANZA UZALISHAJI HIVI KARIBUNI

*Mwenyekiti wa Bodi ya NSSF amesema kitapunguza nakisi ya Sukari nchini

Na: Mwandishi Wetu, Morogoro

Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) chini ya Mwenyekiti wake, Bi. Mwamini Malemi imetembelea mradi wa kiwanda cha sukari Mkulazi kilichopo mkoani Morogoro, ambapo ameahidi kusimamia vizuri mradi huo ili uweze kuleta tija na kurudisha fedha za wanachama.

Aidha, amewahakikishia watanzania kuwa, muda si mrefu kiwanda hicho kitaanza uzalishaji wa sukari ambayo itasaidia kupunguza nakisi ya sukari nchini.

Bi. Mwamini amesema hayo wakati Bodi ya Wadhamini ya NSSF ilipofanya ziara ya kikazi katika kiwanda hicho kinachomilikiwa kwa ubia baina ya NSSF na Jeshi la Magereza.

“Mradi huu ulianzishwa na Serikali kwa lengo la kupunguza nakisi ya sukari nchini, hivyo sisi kama Bodi ya Wadhamini ya NSSF tutahakikisha mradi huu unaleta tija iliyokusudiwa pamoja na kurudisha fedha za wanachama na kupata faida kupitia uwekezaji huu,” amesema Bi. Mwamini.

Amesema mradi wa kiwanda hicho umechangia kuongeza ajira kwa watanzania, kukuza uchumi kwani hayo ndio matarajio ya Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni Hodhi ya Mkulazi, Dkt. Hildelitha Msita, amewahakikishia wanahisa wa kampuni hiyo kuwa, kazi waliyopewa wanaendelea kuifanya na wanakaribia kuimaliza na tayari wameshafanya majaribio ya mitambo yote, na kuwa wako katika hatua za mwisho za majaribio hivyo muda wowote sukari itaanza kuingia sokoni.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mkulazi, Selestine Some, amesema kiwanda hicho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha sukari tani 50,000 kwa mwaka na kitatoa ajira kwa watanzania ambapo mpaka sasa kimeshatoa ajira zaidi 5,000.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here