Home LOCAL HALMASHAURI YA WILAYA TUNDURU YAPOKEA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 1.2 KWA AJILI...

HALMASHAURI YA WILAYA TUNDURU YAPOKEA ZAIDI YA SHILINGI BILIONI 1.2 KWA AJILI YA KUBORESHA MIUNDOMBINU YA SHULE ZA MSINGI.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma akitoa taarifa ya uboreshaji wa miundombinu ya elimu ya msingi ambapo Halmashauri hiyo imepokea zaidi ya Sh.bilioni 1.2 kwa ajili uboreshaji na uimarishaji wa sekta hiyo.

Na Muhidin Amri

Tunduru,

BAADHI ya wanafunzi wa shule ya msingi Ligoma kata ya Ligoma wilayani Tunduru,wameishukuru serikali kupitia Halmashauri ya wilaya kwa kukamilisha ujenzi wa  vyumba 14 vipya vya madarasa na matundu 18 ya vyoo.

Walisema,kukamilika kwa madarasa hayo na uwekezaji wa madawati,kutawawezesha kukaa kwa nafasi,kushawishi wanafunzi wenzao waliokatisha masomo kurudi shule na kuhamasisha kusoma kwa bidii na kutimiza malengo  yao.

Baadhi ya vyumba vipya vya madarasa katika shule ya msingi Ligoma Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma vilivyojengwa kupitia mradi wa Boost.

Fatma Bushir alisema,watayatumia madarasa hayo kufanya vizuri katika masomo yao na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaofaulu na kuchaguliwa kuendelea na masomo ya sekondari.

Jengo la utawala katika shule ya msingi Ligoma wilayani Tunduru.

“tunamshukuru sana mama yetu Rais Dkt samia Suluhu Hassan kutujenga jumla ya madarasa 14 ambayo yatatuwezesha  kukaa darasani kwa nafasi na kuondokana na changamoto ya kukaa wanafunzi wengi katika chumba kimoja”alisema Fatma.

Mwanafunzi mwingine Aziz Hausi alisema,katika shule hiyo kero kubwa ilikuwa msongamano wa wanafunzi kwani darasa moja kuna wanafunzi kati 50  na 60 hivyo kukosa utulivu na umakini wa kusikia wanayofundishwa na walimu wao.

Aidha,ameiomba serikali kuongeza  idadi ya walimu kwani waliopo ni saba tu ambao hawatoshelezi kufundisha wanafunzi zaidi ya 760 waliopo katika shule hiyo inayotajwa kuwa miongoni mwa shule  za msingi zenye idadi kubwa ya wanafunzi wilayani Tunduru.

Mwalimu wa zamu Ibrahim Mapunda alisema,awali shule hiyo ilikuwa na majengo mengi chakavu kutokana na kujengwa kwa muda mrefu, hivyo uwepo wa madarasa mapya kutaongeza ari kwa walimu katika suala zima la ufundishaji wa watoto madarasani.

Alisema,madarasa hayo 14 yataifanya shule hiyo kuwa na mikondo miwili kwa kila darasa,hivyo kupunguza msongamano mkubwa wa watoto uliokuwepo hapo awali ambapo walimu walilazimika kutumia nguvu kubwa katika ufundishaji.

Mapunda,ameishukuru serikali kwa kutoa fedha hizo zilizowezesa kujenga madarasa hayo,hata hivyo ameiomba  kuwajengea nyumba za kisasa ili waondokana na kero ya kupanga nyumba kwa wenyeji ambazo ni chakavu na hazina sifa ya kuishi mtumishi wa umma.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya Tunduru Chiza Marando alisema,serikali imetoa jumla ya Sh.bilioni 1,224,600,000 kwa ajili ya  uboreshaji wa miundombinu ya shule za msingi ikiwemo  shule ya Ligoma iliyopata Sh.milioni 500,132,000 zilizotumika kujenga madarasa 16,matundu ya vyoo 18 na jengo la utawala.

Alitaja shule nyingine zilizopata mgao wa  fedha hizo ni pamoja na shule ya  msingi Tinginya Sh.milioni 331,600 kwa ajili ya kujenga madarasa saba,matundu ya vyoo 14, jengo la utawala na kichomea taka na shule ya Mchangani imepata Sh.milioni  66.3 zilizotumika kujenga madarasa mawili ya awali,na matundu ya vyoo sita.

Alisema,shule ya msingi Mtina imepata Sh.milioni 130,200,000 zilizowezesha kujenga madarasa matano,matundu ya vyoo sita,shule ya msingi Mnazi mmoja Sh.53,100,000 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili na matundu ya vyoo matatu.

Kwa mujibu wa Marando,shule ya msingi Mapinduzi iliyopo kijiji cha Lukumbule imepata Sh.milioni 77,100,000 kwa ili kujenga madarasa matatu na matundu ya vyoo matatu na shule ya msingi Mkasale imepokea Sh.milioni 53,100,000 kwa ajili ya madarasa mawili na matundu ya vyoo matatu.

Alisema,madarasa na matundu ya vyoo katika shule hizo yamekamilika na yataanza kutumika mara shule zikapofunguliwa mwezi Januari mwakani na amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia Halmashauri hiyo fedha za kutosha zilizowezesha kujenga na kuboresha miundombinu ya shule za  msingi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here