Home BUSINESS BRELA YASHAURIWA KUHAMASISHA URASIMISHAJI BIASHARA MBEYA 

BRELA YASHAURIWA KUHAMASISHA URASIMISHAJI BIASHARA MBEYA 

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imeshauriwa kuweka kambi mkoani Mbeya ili kuhakikisha kuwa wafanyabiashara mkoani humo wanarasimisha biashara zao kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.

Ushauri huo umetolewa leo tarehe 22 Desemba, 2023 na Katibu Tawala wa Jiji la Mbeya Bw. Lodrick Mpogoro, wakati akizungumza na Maafisa wa BRELA walipofika ofisi kwake kutoa taarifa ya ziara waliyoifanya mkoani humo ambayo ililenga kutoa elimu kuhusu uwasilishaji wa taarifa za Wamiliki Manufaa wa Kampuni.

Bw. Mpogoro amesema kuwa Jiji la Mbeya linazidi kukua kibiashara hivyo ni vyema BRELA ikaweka kambi ya kurasimisha biashara na kutoa elimu ili wafanye biashara iliyo rasmi na kutambulika na mamlaka mbalimbali.

Pia ameongeza kuwa Mkoa wa Mbeya utawasilisha mwaliko BRELA ili ishiriki katika vikao maalumu vya jiji na halmashauri na kuwawezesha watumishi wa mkoa huo kuwa na elimu kuhusu BRELA na kuifikisha elimu hiyo kwa wananchi.

“Nilipata taarifa ya ujio wenu hapa niwapongeze kwa zoezi hili ambalo mmeliendesha, ninawaomba mfikishe ombi letu kwa Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, kuwa tunawahitaji mrudi hapa na kuweka kambi, ili wafanyabiashara wengi zaidi wasajili biashara zao, “ ameongeza Bw. Mpogoro.

Ameongeza kuwa wafanyabiashara wengi hawajasajili majina ya biashara wala Kampuni kwakuwa hawana elimu ya namna ya kutumia mfumo wa Usajili wa njia ya Mtandao (ORS), hivyo kwa kuweka kambi maalum itasaidia wadau na wafanyabiashara wengi kusajili.

Aidha ameongeza kuwa ili kuongeza idadi ya wafanyabiashara waliorasimisha biashara zao mkoani humo, mkoa utatoa mialiko kwa BRELA kushiriki katika makongamano mbalimbali ili kuchochea elimu ya urasimishaji Biashara.

Ziara elimishi ya BRELA iliyoanza tarehe 18 Desemba na kuhitimishwa leo imehamasisha uwasilishaji wa taarifa za Wamiliki Manufaa wa Kampuni sambamba na kutoa elimu ya urasimishaji wa biashara kupitia usajili wa Kampuni na Majina ya Biashara na kuwakumbusha kuwasilisha taarifa za mwaka kwa kampuni zilizosajiliwa na pamoja na kulipia ada za utunzaji wa Majina ya Biashara.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here