Home BUSINESS WATUMISHI BRELA WAPIGWA MSASA

WATUMISHI BRELA WAPIGWA MSASA

Watumishi wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), wamembukushwa kuzingatia maadili mahala pa kazi ili kufanya kazi zenye kuleta matokeo chanya kwa jamii wanayo ihudumia na taifa kwa ujumla.

Hayo yameelezwa leo Novemba 25, 2023 katika mafunzo kuhusu Maadili ya Utumishi Umma, Kuzuia na Kupambana na Rushwa pamoja na masuala ya Usalama Mtandaoni yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Taifa Cha Utalii, Jijini Dar es Salaam.

Akiwasilisha mada kuhusu vyanzo na rushwa kazini Mchunguzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kumbana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Ilala Bi. Theopista Nalayaga amesema uwajibikaji na kutoa huduma bila upendeleo ni moja ya njia zinazoweza kuzuia mianya ya rushwa kazini.

Aidha ameongeza kuwa mmomonyoko wa maadili, wananchi kutofahamu haki zao, tamaa, ubinafsi, upungufu wa wafanyakazi, na kutokuwajibika kunasababisha kuwepo kwa mianya ya kutoa na kupokea Rushwa.

“Rushwa ina mnyororo wake hivyo tukikumbushana hapa kunasaidia watumishi kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na kuepuka kujihusisha na masuala ya rushwa,” amesema Bi. Nalayaga.

Akizungumza kwa mifano wakili wa Serikali Mwandamizi Kutoka TAKUKURU mkoa wa Ilala Bi. Gloria Mwainyekule amesema kuwa watumishi wa BRELA wanapaswa kuzingatia maadili ili kuepuka makosa ya rushwa yatakayosababisha kuadhibiwa kwa Sheria ya kuzuia na kupambana na Rushwa Sura Namba 329.

“Sheria hii imetungwa mahususi kwa ajili ya kuzuia na kupambana na rushwa, hivyo mienendo ya kutoa na kupokea rushwa moja kwa moja au kupitia mtu mwingine ikibainika, mtumishi anaweza kukabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ambapo adhabu yake si chini ya miaka 20 jela,” amesema Bi. Mwainyekule.

Wakati huo huo maafisa kutoka Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, wamewakumbusha watumishi wa BRELA kuhusu Maadili ya Utumishi wa Umma.

Pia wamekumbushwa kutumia taaluma zao vizuri, pamoja na kuheshimiana, kuwahi kazini, kutoa huduma kwa usawa, kutunza siri za ofisi, na kutenda kazi kwa uadilifu.

Pamoja na hayo Maafisa kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) wametoa elimu kuhusu masuala ya usalama mtandaoni ili kuepusha mambo mbalimbali yanayoweza kujitokeza kwa kutokuzingatia usalama mtandao kama vile kudukuliwa kwa taarifa za ofisi za Umma au kutapeliwa.

Awali akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa Huduma na Uwezeshaji wa BRELA Bw. Daimon Kisyombe amesema BRELA, itaendelea kutoa mafunzo kama haya kwa watumishi ili kuwakumbusha wajibu wao na kuwaepusha na tuhuma za rushwa na ukosefu wa maadili mahali pa kazi.

Pia ameongeza kwa kusema kuwa uongozi unatilia mkazo na kufuatilia malalamiko ya wadau ili kuongeza ufanisi katika toaji huduma kwa kuzingatia Dira na Dhima ya Taasisi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here