Dar. Bohari ya Dawa (MSD), imetwaa tuzo ya Mlipakodi Bora kwa mwaka 2023 ya Mamlaka ya Kodi Tanzania.
Tuzo hizo zimetolewa jana usiku Novemba 24, 2023 katika hafla maalum ya wiki ya Mlipakodi zilizofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City jijiini Dar es Salaam ambako Bohari hiyo imeibuka mshindi wa kwanza katika kipengele cha WalipakodiWalipakodi wa Kati kwa Mkoa wa Kikodi wa Temeke.
Akipokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai amesema ushindi huo una maana kubwa kwa Bohari hiyo na Watanzania .
Amesema MSD ambayo ni moja ya Taasisi za kimkakati za Serikali inayohusika na kuzalisha, kununua, kutunza na kusambaza bidhaa za afya kwa ajili ya vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali nchini inafuata taratibu, sheria na miongozose ikiwa ni pamoja na kulipa kodi stahiki
“Maendeleo yoyote ya nchi yanategemea kodi zinazolipwa hivyo ni vyema kila mlipa kodi akalipa kodi stahiki ili kuwezesha muendelezo wa biashara na kuimarisha maendeleo kwa mustakali wa ustawi wa jamii, “ ameongeza Tukai katika hafla hiyo ambako mgeni Rasmi alikuwa Naibu Waziri Mkuu, Dk Dotto Biteko.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Tukai, MSD sasa iko katika mkakati wa kujiendesha kibiashara hivyo hatua ya kulipa kodi kwa utaratibu uliowekwa hadi kutambuliwa ni fursa ya kuaminika kwa wadau wetu katika huduma tunazotoa.
Awali Mkurugenzi wa Elimu wa Mlipakodi na Mawasiliano, Richard Kayombo alisema vigezo vilivyotumika kupata washindi ni kulipa kiasi kikubwa cha kodi na hiari pamoja na kutunza kumbukumbu vizuri.