Home BUSINESS MRADI WA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI NA USTAHIMILIVU KATIKA NYANDA KAVU...

MRADI WA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIANCHI NA USTAHIMILIVU KATIKA NYANDA KAVU ZA KITROPIKI KUBORESHA UPATIKANAJI WA MAJI DODOMA 

Na: Farida Mkongwe

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Prof. Jamal Katundu amefungua rasmi Warsha ya Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za Kitropiki (CLARITY)  na kusema kuwa anaamini matokeo ya utafiti huo yatasaidia kutatua changamoto zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi pamoja na changamoto za upatikanaji wa maji mkoani Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Prof. Jamal Katundu akifuatilia shughuli zilizokuwa zikiendelea wakati wa kufungua  Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za Kitropiki Kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa maji Jijini Dodoma. (Picha na Tatyana Celestine)

Akifungua Warsha hiyo Oktoba 31, 2023  Prof. Katundu amekishukuru Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kuuchagua mkoa wa Dodoma katika utafiti wao na kusema kuwa kwa takwimu zilizopo Tanzania ina hali nzuri ya upatikanaji wa rasilimali maji zipatazo mita za ujazo bilioni 126 kwa mwaka ambapo mita za ujazo bilioni 105 ni maji juu ya ardhi na ujazo wa bilioni 21 ni maji chini ya ardhi.

“Tafsiri yake ni kuwa katika ardhi kame kama Dodoma nadhani hizo ni takwimu muhimu ambapo wakati mnafanya utafiti itaweza kutusaidia kuja na suluhisho la kutatua changamoto ya maji katika maeneo yaliyo na ukame ikiwemo Dodoma”, amesema Prof. Katundu.

Amesema mkoa wa Dodoma ambao ni Makao Makuu ya nchi umekuwa ukitanuka hivyo basi idadi ya watu pamoja na shughuli za kiuchumi na kijamii zimekuwa zikiongezeka, “ nitumie fursa hii kuishukuru SUA kwa kuiangalia Dodoma na nyie sasa mmekuwa sehemu ya kuisaidia  Serikali kuleta maendeleo ya Dodoma, nina imani utafiti utakaofanyika utatusaidia kupata suluhisho la muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu wa kutatua changamoto ya maji na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa ujumla”. 

Ameongeza kuwa ni fahari kubwa kwa Serikali kuona Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo kimewezesha kupatikana kwa rasilimaji fedha za kuwezesha kufanya utafiti huo lakini pia wanaamini SUA ni miongoni mwa Vyuo shindani ambavyo vitasaidia kutatua changamoto ya maji kupitia mradi huo wa CLARITY na kwamba Serikali ipo pamoja na SUA katika kufanikisha utafiti huo.

Akitoa neno la ukaribisho  kwa niaba ya Makamu Mkuu wa Chuo cha SUA Prof. Raphael Chibunda,  Mkurugenzi wa Utafiti na Uzamili Prof. Ezron Karimuribo amesema SUA imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali kwa kushirikiana na wadau wa ndani na nje ya nchi ili kuongeza nguvu katika kupata majawabu ya changamoto mbalimbali. 

Akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo Prof. Raphael Chibunda, Mkurugenzi wa Utafiti na Uzamili Prof. Ezron Karimuribo akitoa neno la ukaribisho  wakati wa kufungua  Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za Kitropiki . (Picha na Tatyana Celestine)

“Ssi sio kisiwa ni sehemu ya Dunia kwa hiyo tunafanya hivi tukijua wazi kwamba mabadiliko ya tabianchi yakitokea sehemu yoyote ni kwamba yanaweza yakaleta madhara nchini kwetu kwa hiyo ni wajibu wetu kufanya tafiti na ugunduzi wa teknolojia mbalimbali ili ziweze kusaidia katika kutatua changamoto mbalimbali”, amesema Prof. Karimuribo

Amesema changamoto ya mabadiliko ya tabianchi zimekuwa zikijionesha dhahiri katika maeneo mengi nchini hali inayoweza kuwa mbaya zaidi kwenye maeneo ya Nyanda Kavu na Kame za Kitropiki kama ilivyo mkoa wa Dodoma, “SUA imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoukabili mji wetu wa Dodoma hivyo katika Mradi huu wa CLARITY SUA inashirikiana na Wizara yako ya kupitia Kituo cha Umahiri katika masuala ya maji katika kutatua changamoto hiyo.

Awali akitoa maelezo kuhusu Mradi wa CLARITY Prof. Japhet Kashaigili ambaye ni Mtafiti Mkuu wa Mradi huo aamesema malengo makubwa ya kuanzishwa kwa Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda za Kitropiki ni kuimarisha Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi katika jamii za Nyanda Kavu na unategemea kuboresha upatikanaji wa maji, kuelewa jinsi mabadiliko ya tabianchi yatakavyoathiri upatikanaji wa maji kwa baadae na matarajio kuhusu  njia za maendeleo kupitia Mradi huo.

Mtafiti Mkuu wa Mradi wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi na Ustahimilivu katika Nyanda Kavu za Kitropiki Prof. Japhet Kashaigili akielezea namna Mradi huo

unavyotegemea kuboresha upatikanaji wa maji Jijini Dodoma. (Picha na Tatyana Celestine)

Ametaja malengo mahususi ya Mradi huo kuwa ni kubaini changamoto na masuluhisho bunifu kupitia utafiti wa kitaalamu katika fani tofauti, kushirikiana na wadau kuunda njia za mageuzi zilizojadiliwa kupitia ushirikiano katika haidrolojia kwa ajili ya ustamilivu wa mabadiliko ya kijamii, kiuchumi na mabadiliko ya tabia nchi. 

Malengo mengine ni pamoja na kuwezesha ujifunzaji wa pamoja na kubadilishana habari au taarifa kwa ushirikiano ambapo amesema malengo ya utafiti huo yanatarajiwa kufanikiwa  kupitia Maabara za Mageuzi ambazo ni nafasi jumuishi ambazo ni salama ambapo wadau, watafiti na wataalam wanakutana pamoja kufanya majaribio kupima na kubadilishana mawazo katika kuzalisha maarifa na kutathmini masuluhisho. 

Akizungumzia matarajio ya utafiti huo Prof. Kashaigili amesema wanatarajia utafiti huo utakuja na masuhisho mbalimbali yanayohusiana na rasilimali ya maji katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi na kwamba matokeo hayo yatafikiwa kwa ushirikiano na wadau mbalimbali watakaoshiriki katika utekelezaji wa mradi huo.

Aidha ameyataja malengo ya Warsha hiyo kuwa ni kuutambulisha Mradi huo wa CLARITY kwa wadau, kusikiliza na kuweka taarifa vizuri juu ya maoni ya wadau hao kuhusiana na malengo makuu pamoja na matokeo ya utafiti,  kujua maeneo ya ushirikiano na kujua jinsi wadau mbalimbali watakavyoshiriki katika utekelezaji wa matokeo ya utafiti huo.

Akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi Dkt. Devota Mosha ambaye ni Mtafiti Msaidizi wa Mtafiti Kiongozi wa Mradi wa CLARITY kutoka SUA amesema anaamini Mradi huo utatoa suluhisho endelevu la changamoto ya maji jijini Dodoma na ameishukuru Serikali kwa kutoa kibali cha Mradi huo pamoja na kuwaamini watafiti hao kutoka SUA. 

Mtafiti Msaidizi wa Mtafiti Kiongozi wa Mradi wa CLARITY Dkt. Devota Mosha  kutoka SUA akielezea Mradi huo utakavyotoa suluhisho endelevu la changamoto ya maji  jijini Dodoma. 

Mradi huo wa Utafiti ni wa miaka 3.5 unatekelezwa na Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa kushirikiana na WELL Labs (Chuo Kikuu cha IFMR Krea, India) pamoja na taasisi za utafiti nchini Uingereza (UCL, IDS Sussex, UoS, Cardiff University, British Geological Survey), Niger (Abdou Moumouni University) na Nigeria (Chuo Kikuu cha Maiduguri) 

Aidha Mradi wa CLARITY unafadhiliwa na Kituo cha Utafiti wa Maendeleo ya Kimataifa (IDRC Canada), Ofisi ya Mambo ya Nje, Jumuiya ya Madola na Maendeleo (FCDO, Uingereza)  chini ya mpango wa Kukabiliana na Hali ya Hewa na Ustahimilivu (CLARE).

Previous articleMAGAZETI YA LEO NOVEMBA 1,2023
Next articleSIMBA SC YASAINI MKATABA WA BILIONI 1.5 NA SBL
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here