Home LOCAL MAJALIWA AAGIZA VYOMBO VYA HABARI KULIPWA MADENI

MAJALIWA AAGIZA VYOMBO VYA HABARI KULIPWA MADENI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ifanye uratibu wa madai ya vyombo vya habari, sambamba na kuweka mfumo endelevu wa kutatua changamoto hiyo pamoja na changamoto nyingine za wanahabari.

“Taasisi zote za Serikali ziandae mpango wa kuhakikisha kuwa madai yote halali yanawekewa utaratibu maalum wa kuyalipa kwa sababu kuacha kulipa madeni haya ni kudhoofisha uchumi wa vyombo vya Habari.”

Ameyasema hayo leo Novemba 13, 2023 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Saba wa Mwaka wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) katika Uwanja wa Ilulu Mkoani Lindi.

Amewasisitiza wanahabari wote wafanye kazi kwa kufuata sheria za nchi na watambue mazingira ya kazi na kuweka tahadhari zote.

Kadhalika, Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kuwataka Wanahabari wahakikishe wananchi wanapata habari zilizo sahihi na zinazohamasisha maendeleo. “Tunawahitaji sana hususan katika kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini.”

Wananchi msiwabughudhi wala kuwashambulia wanahabari wakiwa wanatekeleza majukumu yao. Kuwashambulia waandishi wa Habari ni uhalifu kama uhalifu mwingine.

Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassana inatambua na kuthamini mchango wa vyombo vya habari katika kuitangaza nchi kitaifa na kimataifa pamoja na kuitangaza mitlradi inayotekelezwa na Serikali kwa wananchi.

“Mheshimiwa Rais amenituma niwahakikishie kuwa wakati wote anapotekeleza majukumu yake, anatambua na kuthamini mchango wa vyombo vya habari nchini na anategemea sekta hiyo kuwa na mchango mzuri katika utekelezaji wa majukumu ya serikali nchini.”

Naye, Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Mathew Kundo amesema wizara hiyo imeendelea kuimarisha ushirikiano mzuri uliopo baina ya Serikali na vyombo vya habari nchini.

“Katika kuhakikisha kunakuwa na uhusiano mzuri baina ya Serikali na vyombo vya habari Mheshimiwa Rais, alielekeza kufanyika kwa mapitio kwa sheria zote zilizokuwa na mapungufu na kulalamikiwa na wadau ikiwemo Media Service Act ya mwaka 2016.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ambavyo inavyoshughulikia changamoto mbalimbalia katika sekta ya habari ambazo zimekuwa zikiwasilishwa na jukwaa hilo kwa muda mrefu.

“Leo hatuna malalamiko, ila tuna shukurani kwa namna ambavyo Serikali imefanyia kazi malalamiko na changamoto zetu, sheria kandamizi ambazo tumekuwa tukizipigia kelele muda wote sasa Serikali imezifanyia kazi.” amesema Balile.

Balile amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia kwa utashi wake wa kurahisisha mazingira ya utendaji kazi kwa sekta ya habari.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 980,
41193 – DODOMA.
JUMATATU, NOVEMBA 13, 2023.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here