Kaimu meneja MSD kanda ya Tabora Adonizedeck Tefurukwa akisoma taarifa ya mbele ya Katibu Tawala wilaya ya Igunga Elizabeth Rewegasira katika uzinduzi wa ugawaji wa vyandarua leo katika kiwanja cha Soko la kati Igunga.
Na: MWANDISHI WETU
SERIKALI imesema hatua ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kugawa vyandarua bure kwa wananchi imelenga kutokomeza ugonjwa wa malaria na kuimarisha uchumi.
Hayo yalisemwa jana Mkoani Tabora Wilayani Igunga na Kaimu Meneja MSD kanda ya Tabora Adonizedeck Tefurukwa katika uzinduzi wa ugawaji wa vyandarua vipatavyo 311,324 kwenye vituo 726 vya kupokelea vyandarua ambapo takribani kaya 78,414 zinatarajiwa kugaiwa vyandarua hivyo.
Alisema lengo la Rais Dk. Samia na serikali yake ni kupunguza ugonjwa wa malaria nchini na kuwa na nguvukazi yenye afya njema kwa maslahi ya kijamii na kiuchumi.
“Matumizi ya vyandarua hivyo itapunguza gharama za matibabu kwani unapotumia chandarua utazuia kuugua malaria, hivyo kuongeza pato la familia kwa kuwa na nguvu kazi yenye afya njema,”alisema.
Tefurukwa alisema MSD,kwa niaba ya serikali ndiyo msambazaji mkuu wa bidhaa za afya kwenda kwenye vituo zaidi ya 7,000 vya Umma na vile vya binafsi vilivyoidhinishwa na Wizara ya Afya.
“Bohari ya Dawa tunayo miundombinu wezeshi na uzoefu wa kutosha, hivyo tunatarajia gharama za usambazaji kuwa rafiki zaidi pia kurahisisha upatikanaji wa takwimu katika bidhaa za afya umeongezaeka na gharama za bidhaa hazijapanda, kwa muktadha huu tupo tayari kusambaza vyandarua hivi ndani ya Halmashauri yako ya Igunga,” alisema.
Aliongeza kuwa ili kurahisisha hatua hiyo ya usambazaji , MSD imekodisha ghala moja wilayani Igunga, ambapo itasambaza mpaka katika vituo vya kupokelea vyandarua (Issuing points).
Aliwataka wananchi wa Igunga kwenda katika vituo walivyojiandikisha ili kupatiwa vyandarua, hivyo ili kuungana na Rais Dk. Samia katika kufanikisha mapambano dhidi ya malaria.
Kwa upende wake Katibu Tawala wilaya ya Igunga Elizabeth Rewegasira alisema kuwa wilaya ya Igunga kupitia Serikali kuu imekuwa ikitekeleza afua mbalimbali kukabiliana na ugonjwa wa Malaria na uhamasishaji wa usafi wa mazingira ili kuangamiza mazalia ya mbu.
“Niwakumbushe kuwa mazingira ya mji wetu ni machafu sana, hivyo ninawaomba kila mmoja katika makazi yetu kwa kushirikiana na watendaji, viongozi wa mtaa na Serikali kuhakikisha kila nyumba imefanya usafi wa mazingira, ikiwemo kufukia madimbwi yote kwani mvua zinazoendelea ni chanzo cha mazalia ya mbu waenezao malaria,” alisema Rewegasira.
Amewataka wananchi hao kuvitumia vyandarua hivyo kwa matumizi ya kujikinga na mbu waenezao malaria na si vinginevyo kwani ikibainika kuwa vinatumika vinginevyo ikiwemo kufugia kuku, kutunzia bustani na kuvulia samaki, kinyume na malengo ya Serikali atachukuliwa hatua za sheria.
Naye, Mganga Mkuu wa Hospitali ya wilaya ya Igunga Dk.Lucia Kafumu ameeleza kuwa wanajivunia hatua zinazochukuliwa na serikali katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo ambapo maambukizi yamepungua kutoka asilimia 15 na kufikia asilimia 5.6.
Alisema wilaya wanaendelea na utekelezaji wa mapango wa kuzingatia kanuni za afya na miongozo kwa kujikinga na magonjwa ambukizi na yatokanayo na uchafu, kwani imebainika hospitali ya wilaya ya Igunga inapokea wagonjwa wengi hasa watoto wenye magonjwa hayo.
Nao baadhi ya Wananchi waliopatiwa vyandarua hivyo akiwemo , Just Doto, Serge Mwita, Stephano Shija na Lusia Kulwa wamemshukuru Rais Dk. Samia na kuahidi kwenda kuvitumia ipasavyo.