Home ENTERTAINMENTS AIWAKILISHA VYEMA TANZANIA

AIWAKILISHA VYEMA TANZANIA

Na: Mwandishi Wetu

AMEIWAKILISHA vema Tanzania!Ndivyo unavyoweza kuelezea baada ya mwanamitindo Jasinta David Makwabe(25) kufanikiwa kuingia katika washindi watano bora wa mashindano ya Future Face Global 2023 yaliyofanyika nchini Nigeria.

Jasinta kutoka nchini Tanzania alipata nafasi ya kushiriki kwenye mashindano ya Future Face Global 2023 baada ya kupata nafasi ya kuwaikilisha Tanzania katika mashindano hayo makubwa ya uanamitindo duniani na hatimaye amepata nafasi ya kuingia katika nafasi tano.

Akizungumza baada ya Jasinta kufanikiwa kuwa katika tano bora Future Face Global 2023,Mratibu wa mashindano hayo kwa Tanzania, Mwanamitindo wa kimataifa Millen Happiness Magese amempongeza Jasinta kwa kuiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya Future Face Global yaliyofanyika Novemba 25,2023.

“Jasinta amebahatika kuwa kwenye tano bora ya washiriki wa shindano hilo lililoshirikisha mataifa mbalimbali ya Afrika , na mshiriki aliyeshinda anatoka Gambia. Nampongeza Jasinta kwa kufika hatua hii na nitoe shukrani kwa wote waliotoa ushirikiano wao mkubwa tangu tulivyoanza mchakato mzima wa Tanzania mpaka alikofika,”amesema Millen.

Ametumia nafasi hiyo pia kutoa mwito kwa wazazi wa Tanzania kwamba wakisikia matangazo ya kuhamasisha vijana kuhusu mashindano ya uanamitindo wawaruhusu kwasababu mashindano haya yana heshima kubwa na yanaweza kumbadilishia mtoto maisha yake kuwa maisha mazuri.

Pia anaweza kupata nafasi ya kufanya kazi na wabunifu wakubwa duniani huku akifafanua Jasinta baada ya kuwa katika nafasi tano za mashindano hayo yeye pamoja na washiriki wenzake wamepata mkataba wa mwaka mmoja wa kufanya kazi na uanamitindo.

“Kwa sasa Jasinta anarudi nyumbani na tayari washindi watano wa mwanzo wamepewa mkataba wa mwaka mmoja wa kufanya uanamitindo lakini bado tunauangalia na baada ya hapo tutajua anakwenda wapi.

Ametumia nafasi hiyo kumueleza Jansita kuwa kwa heshima hiyo ambayo ametupatia ya kuingia tano bora ajue hata kama hakushinda lakini nafasi hiyo ni kubwa kwa nchi yetu ya Tanzania na yeye mwenyewe.

“Kama Jasinta anapenda kujiendeleza kwenye uanamitindo basi ile ni nafasi ambayo ameonekana na wadau mbalimbali, hivyo aendelee kusonga mbele kwasababu hawezi jua nani amemuona hapo na aitumie nafasi hiyo vizuri.”

Millen ametoa mwito pia kwa kampuni za Tanzania mbalimbali kuanza kuwatumia vijana wanamitindo na kuwalipa vizuri kwa kazi ambazo wanafanya ili wasikatishwe tamaa.

“Kazi ya uanamitindo ni kazi kama kazi nyingine, kwa hiyo ni vema vijana hawa wakaendelea kupewa nafasi na kampuni zetu za Tanzania .Huu ni wakati muafaka wa kuwapa nafasi vijana.

“Naendelea kuwahamasisha vijana wanamitindo waendelee kuwa na tabia nzuri kwani kama kampuni inataka kuwatumia halafu hawako katika tabia nzuri inakuwa changamoto, hivyo ni lazima waishi katika misingi mizuri ya kimaadili na kulinda brand zao,”amesema Millen.

Amesisitiza pia umuhimu kwa wanamitindo kuwa na wasimamizi wazuri ambao watawasaidia kufikia ndoto zao za kuwa wanamitindo wa kimataifa.

Aidha ametoa shukrani kwa vyombo vya habari vya Tanzania kwa namna ambavyo vimeshiriki kikamilifu kuripoti mchakato wote wa Future Face global 2023 tangu ulipoanza na hatimaye wamefika tamati na mwakani shindano hilo litafanyika tena.

Kwa upande wake Jansita ametumia nafasi hiyo kuwashukuru Watanzania wote waliomuombea na kumpa kila aina ya ushirikiano tangu kuanza kwa mashindano ya Future Face 2023 ngazi ya nchi na kisha wakati wa fainali za mashindano hayo.

Aidha amesema kupitia mashindano hayo amejifunza na kupata uzoefu mkubwa huku akisisitiza kwake kuingia kwenye tano bora ni fursa kubwa huku akifafanua waliongia tano bora wamepewa mkataba wa mwaka mmoja kuanzia Novemba mwaka huu hadi Desemba mwaka 2024.

“Kusema ukweli nilipofika kule nikikuwa Mtanzania peke yangu kama nilivyosema na jumla tulikuwa washiriki kutoka nchi 20. Na bahati nzuri niliingia kwenye tatu bora ingawa walikuwa wanachagua watano bora na mshindi alitokea Gambia.

“Nimerudi nyumbani na hakika nimejifunza lakini tunafahamu katika mashindano lazima mshindi apatikane na kwangu hoja sio kushinda bali kupata Wakala tu wa kusaini nao na ndio kubwa na katika miezi 12 sasa naweza kupata bahati ya kusainiwa kwenye Agency yao na kama ukisainiwa maana yake umeshafanikiwa, hivyo tunasubiri tuone.

” Nakumbuka wakati wa kutangaza matokeo waliokuwepo eneo la tukio walikuwa wakisikika wakipiga kelele kwa kitaja Jasinta lakini ushindi haukuwa kwangu maana kila jambo na wakati wake.”amesema Jansita.

Aidha ametumia nafasi hiyo kumshukuru Mwanamitindo wa kimataifa Millen Happiness Magesse kwa kuandaa shindano hilo upande wa Tanzania na kumsimamia nyakati zote hadi kufika alipo lakini pia mchango wake mkubwa katika kuibua na kuendeleza vipaji vya wanamitindo nchini.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here