Home BUSINESS TANZANIA NA ZAMBIA ZAKUBALIANA KUTATUA CHANGAMOTO ZA KIBIASHARA 

TANZANIA NA ZAMBIA ZAKUBALIANA KUTATUA CHANGAMOTO ZA KIBIASHARA 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah akiwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda Zambia Bi Lillian Bwalya wakitia saini Makubaliano ya kutatua changamoto za kibiashara 8 kati 24 kati ya Tanzania na Zambia wakati wa Mkutano wa Pamoja wa Kujadili Changamoto za Biashara baina ya nchi hizo uliofanyika 09 – 10/10/2023 katika Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani- Tunduma, Songwe. Vikwazo 16 vitatatuliwa kabla ya Disemba 2023. 

Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah akiongoza Mkutano wa Pamoja wa Kujadili Changamoto za Biashara kati ya Tanzania na Zambia uliofanyika 10/10/2023 ngazi ya Makatibu Wakuu katika Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani- Tunduma, Songwe.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo umejumuisha Makatibu Wakuu kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara, Fedha, Uchukuzi, Ujenzi, Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mambo ya Ndani pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Zambia.

Tanzania na Zambia zimekubaliana kutatua changamoto 8 kati ya 24 za kibiashara na 16 zilizobaki zimewekewa utaratibu wa kuzitatua ifikapo Disemba 31, 2023 ili kurahisisha ufanyaji biashara baina ya Tanzania na Zambia ikiwemo kupunguza msongamano wa malori katika mpaka wa Tunduma.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah Oktoba 10, 2023 akiongea na vyombo vya habari wakati wa Mkutano wa Pamoja wa Kujadili Changamoto za Biashara kati ya Tanzania na Zambia uliofanyika 09 – 10/10/2023 katika Kituo cha Huduma za Pamoja Mpakani- Tunduma, Songwe.

Aidha, Dkt. Abdallah amesema nchi hizo zimekubaliana kuwa bidhaa zinazosafirishwa kutoka Tanzania kwenda nchi nyingine kupitia Zambia zikiwa na vibali vyote vinavyohitajika ziruhusiwe kupita nchini humo kwenda nchi husika bila kizuizi kulingana na Makubaliano ya Kibiashara chini ya Shirika la Biashara la Dunia (WTO) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

Vilevile, amezitaka Taasisi zote za umma zinazohusika na utoaji wa huduma kwa wafanyabiashara wa huduma ya usafirishaji baina ya nchi hizo kuhakikisha hawawakwamishi bila sababu za msingi bali kuwasaidia kutatua changamoto zao hususani upatikanaji wa vibali kulingana na Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo katika makubaliano ya kibiashara chini ya Shirika la Biashara la Dunia na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika.

Katika kuhakikisha masuala hayo yanafanikiwa, Dkt. Abdallah ametoa rai kwa wafanyabiashara ya usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kuhakikisha wanapata vibali vyote vinavyohusika kabla ya kuanza safari ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa hizo bila vikwazo na kuzifikisha katika nchi husika kwa wakati.

Katika hatua nyingine ya makubaliano yaliyotiwa saini na pande zote mbili, amesema Serikali ya Tanzania imekubali kufanya mapitio na marekebisho ya Tozo ya Maendeleo ya Reli kama inavyotekelezwa katika Itifaki ya Biashara ya SADC na kuharakisha mchakato wa urazinishaji wa kanuni za usafirishaji ili ziendane na kanuni za usafirishaji zinazotekelezwa katika Eneo Huru la Biashara la Utatu (Tripatite transport regulations).

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda Zambia, Bi. Lillian Bwalya amesema nchi ya Zambia imekubali kutatua changamoto hizo ili kurahisisha na kukuza biashara za mpakani baina ya nchi hizo.

Akitaja baadhi ya makubaliano yaloyotiwa saini baina ya nchi hizo, Amesema, Zambia imekubali kuboresha changamoto za miundombinu ikiwemo upanuzi wa barabara na kutekeleza mfumo wa upatitanaji wa vibali kabla ya kufika mpakani ili kuboresha mtiririko wa magari mpakani na kuondoa msongamano wa magari uliopo mpakani Tunduma.

Aidha, amesema Zambia imekubali kutumia mfumo wa ufuatiliaji wa mizigo kwa njia ya elektroniki unaotekelezwa nchini Tanzania, au kuharakisha mchakato wa ununuzi wa mfumo unaopendekezwa kutumiwa na Mamlaka ya Mapato ya Zambia (ZRA).

Vilevile, Zambia imekubali kuharakisha urazinishaji wa ada na tozo za barabara kwa Dola za Marekani 10 kwa kilomita 100 unaotekelezwa kaitika Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC). Amesema Bi Bwalya

Bi. Bwalya pia amesema Zambia imekubali kuangalia uwezekano wa kutumia mfumo wa kisasa wa ufuatiliaji wa magari barabarani ili kuondoa na kupunguza vizuizi vya ukaguzi barabarani.

Vilevile, Zambia imekubali kutumia Ofisi jijini Dar es Salaam inayotolewa na Serikali ya Tanzania kwa ajili ya Maafisa wa uondoshaji wa mizigo ya Zambia kuanzia Desemba 31, 2023 ili kirahisisha usafirishaji wa mizigo na kuondoa msongamano wa magari mpakani.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi Prof. Godius Kahyarara amesema makubaliano hayo ni muhimu katika kutatua changamoto mbalimnali baina ya nchi hizo hususani katika kupunguza msongamano wa malori katika mpaka wa Tunduma unaopitisha asilimia 80 ya mizigo kutoka Bandari ya Dar es salaam kwenda nchi za kusini mwa Afrika zisizo na bahari.

Kwa upande wa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha (Usimamizi na Uchumi) Bw. Elijah Mwandumbya akishiriki mkitano huo amesema tozo na kodi mbalimbali zitaendelea kupitiwa na kurekebishwa ili kuwezesha sekta binafsi kutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza kutokana na makubaliano hayo ili kukuza biashara na uchumi wa Taifa

Naye Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Luteni Jenerali Mathew Edward Mkingule amesema changamoto zilizoondolewa zitaongeza ufanisi wa utoaji huduma na kukuza ushirikiano wa kibiashara baina ya nchi hizo.

Previous articlePATA MAGAZETI YA LEO OKTOBA 13,2023
Next articleVIJANA WILAYA YA KALIUA WATAKIWA KUTAFUTA MBADALA TATIZO LA NGUVU ZA KIUME
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here