Home BUSINESS TANZANIA KUTAMBULIANA VYETI VYA MABAHARIA NA BARBADOS

TANZANIA KUTAMBULIANA VYETI VYA MABAHARIA NA BARBADOS

Mkurugenzi Mkuu na Msajili wa Mabaharia na Meli wa Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC) Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge pamoja na Msajili Mwandamizi Mkuu wa Mabaharia na Meli wa Barbados Bw. Giovanni Ciniglio wakitia saini Hati ya Makubaliano (MOU) ya kutambuliana vyeti vya mabaharia kati ya nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Barbados jijini London, Uingereza katika ofisi za Ubalozi wa Barbados.

Kupitia Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (TASAC), Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini Hati ya Makubaliano (MOU) ya kutambuliana vyeti vya mabaharia na nchi ya Barbados leo tarehe 03 Oktoba, 2023.

Akizungumza mara baada ya kusaini makubaliano hayo, Mkurugenzi Mkuu wa TASAC na Msajili wa Mabaharia na Meli nchini Bw. Kaimu Abdi Mkeyenge amesema hadi sasa Tanzania imeanzisha mawasiliano na majadiliano na Nchi 34 kwa ajili ya kuingia katika makubaliano ya kutambuliana vyeti vya Mabaharia (Memoranda of Understanding – MoUs) ili kufungua fursa ya ajira kwa mabaharia wetu, lakini pia kuondoa usumbufu wa kushushwa kwa mabaharia wa kitanzania katika meli mbalimbali ambazo zimesajiliwa na nchi ambazo Tanzania haina mkataba nazo.

“Barbados ni moja ya nchi ambazo tulikuwa tumeanzisha mazungumzo kuhusu kutambuliana vyeti na tunashukuru leo hii tumefanikiwa kusaini Hati ya Makubaliano ya kutambuliana vyeti vya mabaharia, hivyo basi, ni dhahiri kuwa sisi tunatambua mabaharia wa Barbados na wao wanatambua mabaharia wetu”, amesema Bw. Mkeyenge.

Nchi nyingine ambazo Tanzania imeshaanzisha mawasiliano na majadiliano ni pamoja na Bahamas, Algeria, Korea ya Kusini, China, Comoros, Cyprus, Misri, Ufaransa, Ghana, India, Iran, Kenya, Liberia, Malta, Marshall Islands, Mongolia, Oman, Palau, Panama, Peru, Qatar, Saudi Arabia, Singapore, Africa Kusini, Sycheles, Uturuki, Umoja wa Falme za Kiarabu, Vanuatu, Vietnam na nchi za Umoja wa Ulaya.

Previous articleCPA. HOSEA KASHIMBA AZINDUA MAADHIMISHO YA YA PSSSF YA WIKI YA KIMATAIFA YA HUDUMA KWA WATEJA NA KUWAUNGANISHA WATEJA WAKE NA KAMPENI YAKE YA UPANDAJI MITI
Next articleMAENDELEO YA JAMII, NACONGO WASHIRIKIANA KUPANDA MITI 300
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here