Home LOCAL MABORESHO YALIYOFANYWA KITUO CHA AFYA LUKOMBE YAPUNGUZA RUFAA ZA WAGONJWA MTWARA

MABORESHO YALIYOFANYWA KITUO CHA AFYA LUKOMBE YAPUNGUZA RUFAA ZA WAGONJWA MTWARA

Zaidi ya Sh361.5 milioni zilizotumika kufanya maboresho ya kuweka vifaa tiba mbalimbali katika kituo cha afya Likombe kilichopo Halmashauri ya Mtwara-Mikindani zimesaidia kupunguza idadi ya rufaa zinazotolewa kwenda hospitali ya mkoa wa Ligula.

Rufaa hizo zilizopungua kwa wastani wa kati ya 60 hadi 70 kwa mwezi mpaka 10 hadi 15 kumetajwa kupunguza mzigo wa wagonjwa ambao walikuwa wakielekezwa katika hospitali hiyo.

Mbali na hilo pia, uwekaji wa vifaa vya kisasa vya kupimia magonjwa mbalimbali kama selimundu katika hospitali ya Mkoa Mtwara Ligula umefanya sasa majibu ya awali ya ugonjwa huo kupatikana ndani ya dakika 8 kutoka zaidi ya saa 24 za awali.

Hayo yalielezwa kwa nyakati tofauti na wataalamu kutoka hospitali hizo baada ya kutembelewa na Bohari ya Dawa (MSD) ili kuangalia namna maboresho mbalimbali yaliyofanyika hususani katika uwekaji wa vifaa vipya kulivyoleta mabadiliko ya kiutendaji.

Akizungumza, Mganga Mfawidhi wa kituo cha afya Likombe, Dk Victor Andrea alisema awali wakinamama wengi wajawazito walikuwa wakipewa rufaa kwenda hospitali ya mkoa ili waweze kupata huduma kwa sababu walikuwa hawawezi kutoa huduma nyingi.

Lakini baadaye waliwezeshwa kupata vifaa kwa ajili ya huduma mbalimbali ikiwemo ya mama na mtoto na ile ya kuhudumia watoto njiti.

“Hii imefanya idadi ya rufaa tunazotoa kwenda hospitali ya mkoa ya Ligula kupungua kwa kiasi kikubwa kwa sababu tunaweza kuwahudumia hapa, wagonjwa wanaoekwenda hospitali ya mkoa sasa ni wale wanaohitaji madatari bingwa pekee,” alisema.

Alisema maboresho hayo yamesaidia pia kupunguza vifo vilivyokuwa vikitokana na ucheleweshaji wa huduma kwa wagonjwa jambo ambalo kwa sasa halipo.

Upande wa upigaji picha za X ray ndiyo kitu pekee ambacho kituo hicho kinategemea hospitali ya Mkoa ya Ligula lakini hilo huenda likaisha hivi karibuni baada ya mashine ya kupiga picha hizo kuwa tayari zimesimikwa kituoni hapo.

“Tunamalizia vitu vidogovidogo na baada ya muda mchache tutaanza kutoa huduma hizi wenyewe,” alisema Dk Andrea.

Maneno yake yaliungwa mkono na wataalamu kutoka hospitali ya mkoa ya Ligula ambao pia wanakiri kuwa maboresho ya vifaa vya kutolea huduma yaliyofanyika katika hospitali hiyo yamesaidia kupunguza mzigo wa kazi.

Hospitali hiyo katika upande wa maabara imefungiwa mashine mbalimbali ikiwemo ile inayofanya ‘full blood picture’ na mashine ya kisasa ya kufanya vipimo vya selimundu.

Yunusu Jumaa ambaye ni mtaalamu wa maabara katika hospitali hiyo alisema uwepo wa mashine ya kisasa ya full blood picture imefanya kipimo hicho kufanyika kwa urahisi tofauti na awali.

“Pia kupima selimundu mashine hii mpya imepunguza muda uliokuwa ukitumika kutoka zaidi ya saa 24 lakini sasa ndani ya dakika 8 wanapata majibu awali,” alisema Jumaa.

Uwepo wa mashine hizo unatajwa kuokoa muda katika upatikanaji wa majibu jambo ambalo linapunguza muda ambao wagonjwa wanasubiri majibu.

Pia mashine hizo zimeunganishwa na mfumo wa kidigitali ambao unatuma majibu moja kwa moja kwa daktari kwa njia ya kompyuta jambo ambalo linatajwa kupunguza makosa ya kibinadamu katika usomaji majibu.

Mbali na vifaa tiba, katika upande wa upatikanaji wa dawa mkoani Mtwara kwa sasa umetajwa kuimarika tofauti na awali.

Kwa mujibu wa Mussa Juma ambaye ni Mfamasia wa mkoa huo alisema kuna baadhi ya maeneo ambayo upatikanaji wa dawa umezidi mahitaji huku uwekezaji wa fedha kwa ajili ya dawa ukitajwa kuwa sababu.

Pia kujipanga kwa Bohari ya Dawa (MSD) juu ya namna wanavyoweza kupata dawa kutoka kwa wauzaji ikitajwa kuwa sababu nyingine.

“Kwa sasa upatikanaji wa dawa ndani ya Mkoa ni asilimia 70 ya mahitaji ya dawa, MSD hawacheleweshi kuleta dawa wanatumia siku chache kuleta dawa jambo ambalo kinafanya upatikanaji wake kuwa wa uhakika,” alisema Juma.

Kuhusu asilimia 30 zilizobakia alisema wamekuwa wakitumia mfumo wa mshitiri ulioruhusiwa na serikali katika kupata dawa zinazobakia ambapo alisema kwa sasa wanao wawili ambapo mmoja hutia huduma ya vifaa tiba na mmoja dawa.

“Tofauti na kipindi cha nyuma, kulikuwa na shida katika huduma tulikuwa tukitumia muda mrefu kupata oda tunazohitaji. Unaweza kufika katika kituo hakuna dawa lakini umeshaomba MSD hujapata, halii hii kwa sasa haipo ukiomba unaopewa ndani ya muda mfupi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here