Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya wafanyabiashara wanawake Tanzania (TABWA), Bi. Noreen Mawalla, akizungumza katika mkutano wa B2B uliowakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na China kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kujenga mahusiano ya Kibiashara. mkutano huo umefnyika usiku wa Octoba 13,2023 Jijini YIWU, nchini China.
Bw. Cosmo Zhang Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Professional Exchange Platform (Pexpla), iliyofadhili safari ya wafanyabiashara hao kwa kushirikiana na TABWA akizungumza alipokuwa akitoa hotuba yake ya ukaribisho kwa wafanyabiashara kutoka Tanzania, kwenye mkutano aliouandaa wa B2B uliowakutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na China katika Jiji la YIWU nchini China.
Mwenyekiti wa TABWA Bi. Jenipha Japhet akitoa salamu zake alipokuwa akizungumza kwenye mkutano huo.
(PICHA NA: HUGHES DUGILO)
Na: Hughes Dugilo, CHINA.
Wafanyabiashara wa Tanzania hususani wanawake wametakiwa kuchangamkia fursa za kibiashara zinazopatikana katika mataifa ya kigeni kwani kwa kufanya hivyo kutaongeza wigo wa masoko na kujifunza mbinu mbalimbali za kibiasahara.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wafanyabiashara Wanawake Tanzaania (TABWA), Bi.Noreen Mawalla, alipokuwa akizungumza kwwenye mahojiano maalum wakati wa mkutano wa ana kwa ana uliowakutanisha pamoja wafanyabiashara wanawake kutoka Tanzania na China, uliofanyika Octoba 13, 2023 katika Jiji la Yiwu nchini China.
Amesema kuwa Mkutano huo ni maalumu kwa wafanyabishara hao kwani umewakutanisha moja kwa moja na wafanyabiashara, pamoja na wazalishaji wa Bidhaa mbalimbali kutoka nchini china ili kubadilishana uzoefu wa kibiashara na kutanua wigo wa soko la bidhaa zao.
“Leo tumekuwa na mkutano wa ana kwa ana kati ya wafanyabiasha wa Tanzania na China ambapo wafanyabiashara takriban wa 40 katika sekta ya Viwanda vya nguo, vifaa vya mashuleni na maofisini, vipodozi, chakula na vyombo wamehudhuria ili kujifunza, lakini pia kuweza kujenga mtandao wa kibiashara.
“Kupitia mkutano huu, wafanyabiashara wameweza kujenga mtandao na mahusiano ya kibiashara, kufanya oda ya bidhaa mbalimbali bila kupitia madalali, kwa sababu wamekutana na wazalishaji wenyewe,” amesema Noreen
Ameeleza kuwa Taasisi hiyo imekuwa na jukumu kubwa la kuwaunganisha wafanyabiashara wanawake kutoka Tanzania na kutafuta fursa mbalimbali za masoko ya ndani na nje ya nchi ili kutimiza malengo yao.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TABWA, Bi. Jenipha Japhet akizungumza katika hotuba yake, ameishukuru Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fursa kwa wanawake, na kuwawezesha kuyafikia malengo yao ya kibiashara, na kwamba amekuwa kinara kwa wanawake kufanikisha ndoto zao na kuwafungulia milango ya kibiashara Duniani.
“Hii timu kutoka Tanzania mimi nikiwa mmoja wapo tunahitaji ushirikiano wenu wa kina ili tuweze kunufaika na hiki kikao na siyo sisi tu kunufaika, bali na nyie mnufaike kuja kufanya biashara Tanzania, kwa lugha nyingine tunasema ‘nipe nikupe’.
“Hii Nipe Nikupe ningependa itumike kama kauli mbiu ya huu mkutano ambapo tunahitaji zaidi kwa jinsi ambavyo tupo hapa kwenu China mtuhudumie vizuri kwa uaminifu ili na nyinyi kesho mkija kwetu Tanzania tuwahudumie vizuri na kwa namna moja au nyingine tusiangalie kupata faida ya leo tu, bali tuangalie pia na kesho”,amesema Bi.Jenipha.
Nae, mfanyabiashara na mwanachama wa TABWA Justina Mutafungwa, amesema kuwa mkutano huo umekuwa na manufaaa makubwa kwa kubadilishana uzoefu na wafanyabiashara wa China katika sekta mbalimbali.
“Kupitia TABWA nawahamasisha wajasiriamali wote wakisikia matangazo kuhusu fursa zinazopatikana China waweze kujitokeza kwa wingi kwa sababu TABWA ni Taasisi ambayo imejikita sana kuwasaidia wanawake wanaopenda kunyanyuka kwenye Biashara” amesema Justina