Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba amewataka waajiriwa wapya wa kada mbalimbali kujiepusha na vitendo vya rushwa ili kuendelea kujenga taswira chanya katika Tume ya Madini na Sekta ya Madini kwa ujumla.
Mhandisi Samamba ametoa rai hiyo leo Septemba 20, 2023 jijini Dodoma kwenye ufunguzi wa mafunzo elekezi kwa waajiriwa wapya wanaotarajia kufanya kazi katika Ofisi za Tume ya Madini zilizopo makao makuu na mikoani.
“Mfahamu ya kuwa Sekta ya Madini ina vishawishi vingi sana, hivyo mnatakiwa kuwa makini kwenye utoaji wa huduma kwa wananchi wanaofika kwenye Ofisi za Madini kwa kutoa huduma kwa kiwango cha ubora wa hali ya juu, ubunifu, uadilifu na bila upendeleo na kuvutia wawekezaji kuwekeza kwenye Sekta ya Madini,” amesema Mhandisi Samamba.
Katika hatua nyingine, Mhandisi Samamba amesema kuwa wananchi wana matarajio makubwa katika Sekta ya Madini, na kuongeza kuwa Tume ya Madini imeweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini kuanzia kwenye utafiti, uchimbaji, uchenjuaji, biashara ya madini, kanuni za ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini ( Local Content) na Wajibu wa Kampuni za Madini kwa Jamii (CSR)