Na: Halfan Abdulkadir, Zanzibar.
Ikiwa Leo Ulimwengu ukiadhikmisha siku ya Demokrasia, Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Ada Tadea ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania Mhe. Juma Ali Khatib amesema kuwa Tanzania imefanikiwa kwa kiwango kikubwa katika kuimarisha demokrasia na siasa hali ambayo imepelekea nchi kuwa katika hali nzuri ya Utawala Bora ukilinganisha na nchi nyengine za Barani Afrika.
Hayo ameyasema mapema leo Septemba 15,2023 wakati alipokutana na uongozi wa Taasisi ya Mpango wa hiyari wa nchi za umoja wa Afrika kujipima katika vigezo vya utawala Bora (APRM Tanzania) katika Ofisi za Baraza la Wawakilishi Chukwani Zanzibar.
Mhe Juma amesema kuwa katika uso wa dunia Tanzania ina taswira nzuri na kubwa kuhusu masuala ya Utawala Bora na hilo linatokana usimamizi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuonesha ukomavu wa hali ya juu katika siasa kwa kufungua milango ya demokrasia na kuruhusu mikutano ya hadhara ya Kisiasa.
Aidha ameahidi uongozi wa APRM Tanzania kuwa yeye pamoja na wafuasi wa Chama cha Ada Tadea wapo tayari kutoa ushirikiano kwa APRM wakati ambapo wataalamu wa kukusanya maoni wakifika katika maeneo yao.
Kwa upande wake Katibu mtendaji wa APRM Tanzania Lamau Mpolo amesema kuwa vyama vya Siasa ni wadau muhimu kwa APRM na watahakikisha kuwa maoni na michango yao inachukuliwa kwa uzito mkubwa katika uandishi wa Ripoti ya Pili ya Tathmini ya masuala ya Utawala Bora Tanzania.
Lamau ameongeza kuwa kwa vile dhumuni la APRM Tanzania ni kukuza dhana ya Utawala Bora kwa kuzingatia vigezo vinavyokubalika kimataifa hivyo itahakikisha inafuata msingi wa kuwashirikisha wananchi bila kutumika kisiasa ili iweze kuandaa Ripoti ambayo itakubalika Kimataifa na kuweza kuharakisha shughuli za kimaendeleo pamoja na kuimarisha muungano wa kikanda na Bara zima la Afrika.
Siku ya Demokrasia Duniani huadhimishwa ifikapo September 15, ya Kila mwaka, ambapo lengo Kuu la siku hiyo kutathimin na kuchagiza Demokrasia katika Mataifa mbalimbali Ulimwenguni.