Home BUSINESS TANTRADE YAIPA KONGOLE MKOA WA GEITA KWA MAONESHO YALIYOFANA

TANTRADE YAIPA KONGOLE MKOA WA GEITA KWA MAONESHO YALIYOFANA

Afisa Biashara wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), Bi. Samirah Mohamed, akizungumza alipokuwa akitoa salamu za Taasisi hiyo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE Bi. Latifa Khamisi, katika hafla za kuhitimishwa kwa Maonesho ya sita ya Teknolojia ya Sekta ya Madini yaliyofungwa rasmi leo Septemba 30,2023 na Makamu wa Pili Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hemed  Suleiman, katika viwanja vya EPZ Bombambili Mkoani Geita.

(PICHA NA: HUGHES DUGILO)

Na: Hughes Dugilo, GEITA

Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE), imeupongeza Uongozi wa Mkoa wa Geita kupitia Halmashauri ya Mji Geita kwa kuiamini Taasisi hiyo na kuitambua kama chombo pekee cha Serikali chenye Mamlaka ya kuratibu na kudhibiti Maonesho yote yanayoandaliwa nchini.

Hayo yameelezwa na Afisa Biashara wa TANTRADE Bi. Samira Mohamed alipokuwa akitoa salamu za Taasisi hiyo, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TANTRADE Bi. Latifa Khamisi katika hafla ya kuhitimishwa kwa maonesho ya sita ya Teknolojia ya Sekta ya Madini yaliyofungwa rasmi leo Septemba 30,2023 na Makamu wa Pili Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Hemed  Suleiman, katika viwanja vya EPZ Bombambili Mkoani Geita.

Samira amesema kuwa imani hiyo imepelekea kuanzishwa kwa makubaliano (MoU) ya kukuza Maonesho hayo, ili yaweze kufikia viwango vya kitaifa na kimataifa.

Amesema kuwa Taasisi hiyo imeshiriki kikamilifu kwenye maonesho hayo ikiwa ni miongoni mwa wajumbe katika Sekretarieti ya maandalizi huku ikiratibu na kusimamia Kliniki ya Biashara yenye jukumu la kutoa huduma kwa pamoja, kusikiliza na kutatua changamoto za wadau na wananchi mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara.

Akizungumzia Kuhusiana na Maonesho ya Kimataifa ya wenye viwanda yajulikanayo kama Tanzania International Manufacturers Expo (TIMEXPO), Bi Samira amesema kuwa maonesho hayo yanatarajiwa kuanza rasmi tarehe 4 hadi 6 Oktoba, 2023, Jijini Dar es Salaam, na kwamba wananchi wote na wadau mbalimbali wanakaribishwa kutembelea.

Ameongeza kuwa TANTRADE, pia iko kwenye uratibu wa ushiriki wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika Maonesho ya Kilimo (Horticultural Expo) ya Doha – Qatar yanayotarajiwa kufunguliwa rasmi tarehe 2 Oktoba, 2023, ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amealikwa katika ufunguzi huo.

“Maonesho hayo ya Expo 2023 Doha yatafikia kilele tarehe 28 Machi, 2024, hivyo Washiriki wa Maonesho haya na watanzania wote mnakaribishwa kushiriki” ameongeza.

Amewakaribisha wananchi na wadau wote, kutembelea katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), 2024 maarufu Sabasaba, yanayofanyika kila mwaka kuanzia tarehe 28 Juni hadi 13 July.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here