Home BUSINESS TAASISI ZA UDHIBITI ZAELEZWA KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI YA UFANYAJI BIASHARA NCHINI

TAASISI ZA UDHIBITI ZAELEZWA KUWEKA MAZINGIRA WEZESHI YA UFANYAJI BIASHARA NCHINI

Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dkt. Hashil Abdallah, akizungumzia alipokuwa akifunga kikao kazi kilichohudhuriwa na Taasisi za Udhibiti leo tarehe 15 Septemba, 2023 Mkoani Morogoro.

Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa akizungumza katika kikao kazi hicho kilichofanyika Mkoani Morogoro

MOROGORO

Taasisi za Udhibiti zimeelekezwa kuweka mazingira wezeshi ya ufanyaji biashara nchini ikiwa ni jukumu kuu na la msingi ili kutatua kero za wafanyabiashara na wawekezaji kwenye sekta mbalimbali badala ya kuwa kikwazo na endapo kuna sheria, kanuni na taratibu zenye mikinzano zirekebishwe.

Wito huo umetolewa na Dkt. Hashil Abdallah, Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, alipokuwa akifunga kikao kazi kilichohudhuriwa na Taasisi za Udhibiti leo tarehe 15 Septemba, 2023 Mkoani Morogoro ambapo kikao hicho kiliratibiwa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).

Dkt. Abdallah amesema kuwa Taasisi za Serikali zinatakiwa kuzungumza kimifumo hasa katika maeneo yanayohusiana kiutendaji ili kumsaidia ambaye anataka kufanya baishara au kuwekeza nchini na kupata huduma kwa kasi kwakuwa uchumi wa nchi unakuwa kwa kutegemea mazingira bora ya ufanyaji biashara nchini na kuchochewa kuanzia ngazi ya Taasisi.

Ameongeza kwa kusema kuwa mageuzi hayo yanayofanywa na Serikali, yanalenga pia kuwawezesha wazalishaji wa bidhaa na wafanyabiashara kuzifikia fursa mbalimbali za masoko ya Kikanda na Kimataifa ili kukuza mauzo ya nje na kuiwezesha nchi kuongeza wigo wa ajira na fedha za kigeni.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa, amemuhakikishia kuwa BRELA itawasilisha rasmi Wizarani maazimio yote ya kikao ili hatua mbalimbali zichukuliwe katika maeneo ambayo yanahitaji uboreshaji na kufikiwa maamuzi kwa haraka.

BRELA imekutana na Taasisi za Udhibiti ili kujadili mikakati ya pamoja ya namna ya kutatua mikinzano inayojitokeza katika utendaji kazi wa kila siku, kutokana na Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia Taasisi hizo hapa nchini, Kikao kazi hicho kilianza tarehe 13 Septemba, 2023 hadi 15 Septemba, 2023.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here