Home BUSINESS SINOTAN YAANZA KULETA MAPINDUZI YA VIWANDA KWALA

SINOTAN YAANZA KULETA MAPINDUZI YA VIWANDA KWALA

 Na: Selemani Msuya, Kibaha

SERIKALI imesema uwekezaji unaofanywa na Sino-Tan katika Kongani ya Viwanda iliyopo Kwala, wilayani Kibaha mkoani Pwani utafanikisha ujenzi wa viwanda 200 vitakavyogharimu zaidi ya shilingi trilioni 8 hadi kukamilika kwake mwaka 2025.

Aidha, Serikali imesema pindi viwanda hivyo vikikamilika vitafanikisha Watazania 100,000 kupata ajira, huku mapato zaidi ya shilingi trilioni 1.3 yakipatikana kwa mwaka.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo wakati alipotembelea kongani hiyo akiwa ameambatana na wawekezaji na wafanyabiashara zaidi 120 kutoka jimbo la Zhejiang nchini China ambao wamekuja kuona namna Tanzania inaendeleza sekta ya viwanda na fursa zilizopo.

Waziri Kitila amesema Rais Samia Suluhu Hassan amedhamiria kujenga Tanzania ambayo ina uchumi shirikishi wa viwanda, hivyo kinachofanywa na Sino Tan ni utekelezaji wa ndoto ya rais.

Alisema uwekezaji huo ni itekelezaji wa dira ya Rais Samia ya uwekezaji aliyoiahidi Aprili 22, 2021 alipolihutubia Bunge la Jamhuri ya Muungani jijini Dodoma na ni jambo jema kuwa Sino Tan imeunga mkono kwa vitendo.

“Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia imeamua kuvutia wawekezaji kwenye sekta zote ikiwemo ya viwanda, hivyo ujio wa Sino Tan ni mwanzo mzuri, kwani 2025 tutakuwa na chakuwaambia wananchi katika eneo hilo muhimu kwa uchumi wa nchi. Viwanda 200 na ajira 100,000 sio jambo dogo, tunaenda kuibadilisha Kwala. Naomba Watanzania waje kuwekeza katika eneo hilo muhimu,”alisema.

Profesa Kitila alisema kongani hiyo ya viwanda yenye ukubwa wa hekari 2,500 ni ya kwanza kwa ukubwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki na ya nne Afrika hivyo ni wazi inaenda kukuza uchumi wa nchi kwa kasi kubwa.

Waziri huyo alisema uwekezaji huo wa awali unagharimu zaidi ya Shilingi bilioni 880 na ukikamilika kwa kujenga viwanda zaidi ya 200 zaidi ya shilingi trilioni 8 zitakuwa zimetumika.

Alisema mikakati ya wizara yake na ile ya Viwanda na Masoko ni kuhakikisha Tanzania inakuwa na kongani nyingi za viwanda ambazo zitawezesha kukuwa kwa uchumi kwa haraka.

Waziri Kitila alisema kongani hiyo itahusisha viwanda vya nguo ambapo wakulima wa pamba kutoka mikoa 17 watanufaika na nchi kuondokana na uuzaji wa pamba nje ya nchi kwa asilimia 80.

Prof. Kitila alisema pia kutakuwa na viwanda vya kutengeneza viatu, hivyo itakuwa ni fursa kwa wafugaji wa Tanzania ambapo inadaiwa Tanzania ipo katika nchi tano bora kwa wingi wa mifugo.

“Kongani hii itakuwa na kiwanda kikubwa cha dawa, katika Bara la Afrika, pia kiwanda cha kemikali mbalimbali, kusema kweli Sino Tan inaenda kuifungua Tanzania kiuchumi,”alisema.

Alisema mipango ya serikali ni kuhakikisha asilimia 100 ya dawa zinapatikana nchini, hali ambayo itakuza uchumi na kuchochea maendeleo.

“Asilimia 80 ya dawa zinaagizwa nje ya nchi, hali ambayo inasababisha nchi kukosa fedha za kigeni, ila ujio wa viwanda hivyo nchi itakuwa na fedha nyingi za kigeni,” alisema.

Kitila alisisitiza kuwa ujenzi wa viwanda hivyo unaenda kuteka soko la Afrika ya Kati, Mashariki na Kusini na kuziomba nchi za ukanda huo kutumia bidhaa za Tanzania.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe alisema ujenzi wa viwanda hivyo unaendana na ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo inazungumzia kuongeza ajira kwa makundi yote.

Kigahe alisema wizara hiyo itatoa ushirikiano kwa mdau yoyote ambaye anataka kuwekeza katika sekta hiyo na iwapo kutatokea vikwazo watoe taarifa kwa viongozi.

“Rais Samia anataka viwanda viongezeke, hivyo hatupo tayari kuona mwekezaji anakwambishwa, tutachukua hatua kwa yoyote anayekwamisha dhamira ya kiongozi wetu wa nchi,”alisema.

Mwenyekiti wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Dk Binilith Mahenge alisema mradi huo ulisajiliwa Julai 30, 2021 na umechukua eneo la ekari 2,500 na zilizoanza kuendelezwa ni ekari 500 na matarajio yao ni ifikapo 2025 viwanda vyote viwe vimejengwa.

Alisema TIC inaendelea kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwenda kuwekeza katika kongani hiyo ambayo ina sifa za kimataifa.

“Hapa Kwala kuna huduma zote, muhimu kama reli, barabara na viwanda, hivyo nitumie nafasi hii kuwashawishi wawekezaji kuja kuwekeza ili waungane na Sino Tan,” alisema

Alisema awali kulikuwa na changamoto ya kupata vivututio vya uwekezaji lakini chini ya uongozi wa Rais Samia vivutio vimewekwa, hivyo kuwataka wawekezaji kuja Tanzania kuwekeza.

Naye Mwenyekiti wa Sino Tan, Janson Huang alisema wameamua kuwaleta wawekezaji na wafanyabishara kutoka China kuja kuona fursa zilizopo nchini, ili nao waweze kuchangia uchumi wa nchi hiyo.

Huang alisema Tanzania ni nchi yenye amani, umoja na upendo, hivyo ni imani yake wawekezaji na wafanyabishara hao watavutiwa kuwekeza nchini.

“Sisi tunaamini Tanzania ni sehemu sahihi ya uwekezaji na kufanya biashara, hivyo ndugu zetu hawa wameona hapa Kwala kinachofanyika naamini watakuja kuwekeza na nchi zetu zinanufaika, “alisema.

Mwenyekiti huyo alisema matarajio yao ni kuona viwanda vitakavyojengwa katika eneo la Kwala vinaenda kutoa huduma katika nchi za Afrika.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here