Home LOCAL RAIS SAMIA KUFANYA ZIARA YA KIHISTORIA MTWARA, LINDI

RAIS SAMIA KUFANYA ZIARA YA KIHISTORIA MTWARA, LINDI

Na: Mwandishi Wetu, Mtwara
 
Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara kwenye mikoa ya Mtwara na Lindi kuanzia tarehe 15-20 Septemba, 2023. 
 
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, katika ziara hiyo ya mikoa ya kusini, Rais Samia atazindua na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo.
 
Kama ilivyo desturi ya uongozi wake wa kuwajali wananchi wa chini, Rais Samia pia atasikiliza kero na matatizo ya wananchi kwenye maeneo yote atakayotembelea.
 
Pamoja na mambo mengine, Rais Samia atazindua Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini wakati wa ziara yake ya mkoa wa Mtwara.
 
Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini iliyopo Mikindani Mkoa wa Mtwara ulianza mwaka 2021.
 
Hospitali hiyo kubwa na ya kisasa itahudumia mamilioni ya wakazi wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.
 
Ujenzi wa hospitali hiyo unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni 15.8.
 
Tangu alipoingia madarakani mwezi Machi 2021, Rais Samia amefanya uwekezaji mkubwa kwenye sekta ya afya ambao haujawahi kutokea tangu Tanzania ipate uhuru miaka 62 iliyopita.
 
Katika ziara yake ya mikoa ya kusini, Rais pia atazindua Chujio la Maji Mangamba na atakagua ujenzi wa uwanja wa ndege, pamoja na kuzindua barabara za mkoa wa Mtwara.
 
Mikoa ya Lindi na Mtwara inatoa mchango mkubwa kwenye uchumi wa Tanzania na ni maarufu kwa kilimo cha korosho, shughuli za uvuvi na rasilimali ya gesi asilia.
 
Serikali inaendelea kufanya uwekezaji mkubwa kwenye bandari ya Mtwara, huku jitihada zikiendelea kukamilisha uwekezaji wa kampuni binafsi za kimataifa wa Dola za Marekani takribani bilioni 40 (sawa na zaidi ya shilingi trilioni 100) kwenye mradi mkubwa wa kuchakata gesi asilia (LNG) mkoani Lindi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here