Home BUSINESS RAIS SAMIA AIPONGEZA OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI KUVUTIA WAWEKEZAJI NA...

RAIS SAMIA AIPONGEZA OFISI YA RAIS, MIPANGO NA UWEKEZAJI KUVUTIA WAWEKEZAJI NA KUWEKA MAZINGIRA BORA YA UWEKEZAJI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji na Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kuweka mazingira bora ya Uwekezaji pamoja na kuvutia wawekezaji.

Rais Samia ametoa pongezi hizo, Septemba 20, 2023 kwenye hafla ya uzinduzi wa Kiwanda cha Uzalishaji Vioo vya Ujenzi cha Saphire Float Glass kilichopo wilayani Mkuranga, mkoani Pwani.

“Nawapongeza Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Kituo cha Uwekezaji (TIC) kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wanaokuja nchini kuwekeza, hali hii ya uwekezaji hapa nchini inachochea ukuaji wa uchumi wetu pia inachagiza ajira nyingi kwa vijana wetu,” amesema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia ameeleza kuwa hadi kufika Septemba, 2023 Kituo hicho cha Uwekezaji (TIC) kimesajili jumla ya miradi 417 katika Sekta ya Viwanda kati ya Januari 21 na Septemba 15, 2023. Miradi hiyo ina jumla ya thamani (USD) Bilioni 5 na Milioni 39 sawa na wastani wa Shilingi Trilioni 12 za kitanzania, ikiwa kila mradi umegharimu wastani wa (USD) Milioni 12.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo amesema Kiwanda hicho kitaleta mapato mapya ya Kodi takribani Shilingi Bilioni 42.79 kila mwaka sanjari na kuleta ajira nyingi kwa Watanzania wengi kutoka sasa kwenye ujenzi wake ambapo zaidi ya watu 700 wamepata ajira kwenye ujenzi wa mradi huo.

Naye, Waziri wa Viwanda na Biashara nchini, Dkt. Ashantu Kijaji amesema kupitia uongozi mahiri wa Rais wa awamu ya sita, Dkt. Samia, Wawekezaji wa Kiwanda hicho walikubali kuwekeza nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni inayojenga mradi huo, Frank Yang ameishuru Serikali ya Tanzania na watu wa Tanzania kwa ukarimu wao wakati wote wa ujenzi wa Kiwanda hicho cha vioo katika eneo hilo la Mkuranga, Pwani.

Mradi huo wa Kiwanda cha Vioo ni mradi mkubwa tangu kusajiliwa kwa miradi hiyo nchini ukiwa umegharimu fedha za Marekani (USD) Milioni 311 sawa na wastani wa Shilingi Bilioni 745 na zaidi ya Milioni 700, Kiwanda hicho ni kikubwa zaidi ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, kikiwa nafasi ya nne Afrika.

Kiwanda hicho cha Vioo kinatarajiwa kuzalisha Tani 700 za Vioo kwa siku katika uzalishaji kamili, awamu ya kwanza. Asilimia 75% ya bidhaa zitauzwa nje ya nchi wakati asilimia 25% za bidhaa hiyo zitauzwa nchini. Pia Kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha ajira takribani 1650 kwa vijana wa kitanzania.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here