Na: Halfan Abdulkadir, ZANZBAR
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amewakata Watanzania waliokabidhiwa vyeti vya Uraia wa Kuandikishwa (Tajnisi) kuendeleza utiifu wa sheria na kujiepusha na vitendo viovu ili wasipotoshe dhamira njema ya Serikali ya kuwapa uraia wa Tanzania.
Dk. Mwinyi alitoa kauli hiyo Ikulu, Zanzibar alipokabidhi vyeti hivyo kwa Watanzania 3,319, wahamiaji wasiohamishika baada ya kikidhi vigezo na Sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa raia halali nchini.
Rais Dk. Mwinyi aliwataka Watanzania hao kuipa heshima inayostahili hadhi waliyopewa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuwa raia, kwa kuwa raia wema na wenye kulitakia mema Taifa.
“Kwa hakika ndugu zangu mna wajibu kwa pamoja tushirikiane kulinda na kudumisha amani tuliyonayo kwa faida yetu, tuliopo sasa na wale watakaokuja baadae” aliwaasa Watanzania hao.
Rais Dk. Mwinyi aliwahakikishia Watanzania hao kuwa na haki zote baada ya kuthibitishwa uraia wao kama wanazostahili raia wengine wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pia, aliwaasa kuzitumia vema haki na fursa hizo kwa kushiriki kikamilifu kwenye harakati za maendeleo kwa ustawi wa familia zao na Taifa kwa jumla na kuwataka ambao hawajajisajili kufanya hivyo kwa mamlaka husika.
“Natumia nafasi hii kutoa wito kwa ndugu zetu ambao kwa namna moja au nyengine hawajafika kwenye Ofisi za Uhamiaji kujiorodhesha, ni vyema wakaitumia fursa hiyo ili watambuliwe rasmi, Serikali zetu zimedhamiria kulimaliza tatizo hili kutokana na athari zake”. Aliwasihi Dk. Mwinyi.
Sambamba na kuzitaka mamlaka za Serikali na Binafsi kuwapa ushirikiano Watanzania hao kwenye masuala mbalimbali kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na miongozo iliyopo kama wanavyofanyia Watanzania wengine.
Katika hatua nyengine Rais Dk. Mwinyi alitoa wito kwa Idara ya Uhamiaji, kuendelea kuziimarisha sheria zilizopo hususan Sheria ya uraia wa Tanzania kwa kuifanyia mapitio kwa madhumuni ya kuiwezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowahusu wananchi na wageni wanaofika nchini.
Naye Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni Yussuf,alizipongeza Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa busara zao za kuwasamehe Watanzania hao malipo ya shilingi milioni mbili kulipia uraia wao pamoja na kupongeza ushirikiano kwa Serikali mbili hizo kulifanikisha jambo hilo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi, Hamza Hassan Juma alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kukamilisha ahadi ya kuzitatua changamoto za Wanzania hao wahamiaji wasiohamishika tangu alipowaahidi mwaka 2020 kuitekeleza kwa vitendo ahadi yake ya kushughulikia changamoto za Watanzania hao.
Kwa upande wake, Kamisha Jeneral wa Uhamiaji Tanzania, Dk. Anna Makakala alisema jeshi hilo linajukumu la kuratibu masuala yote ya uhamiaji nchini yanayohusu raia wanaoomba uraia kisha kukabidhi kwa Waziri wa Mambo ya ndani ya nchi.
Aidha alieleza Idara ya Uhamiaji Zanzibar kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilifanya zoezi la utambuzi kwa Watanzania hao mara baada ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Watanzania hao waliokuwa wakikabiliwa na changamoto za kukosa haki zao za msingi kisheria zikiwemop hati za uraia, hati za kusafirikia na haki nyengine wanazopatiwa Watanzani halisi.
Jumla ya Watanzania 3319 wenye asili ya mataifa mbalimbali waliokua wahamiaji wasiohamishika wametambuliwa rasmi na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa raia halali wa Tanzania. Miongoni mwao 3116 wanaasili ya Msumbiji, 147 wanaasili ya visiwa vya Komorao, watano kutoka Burundi na raia mmoja kutoka Jamhuri ya Rwanda, aidha watoto 1675 pia walitambuliwa.