Home LOCAL KINANA ATANGAZA HATARI KWA WANAONYATIA MAJIMBO

KINANA ATANGAZA HATARI KWA WANAONYATIA MAJIMBO

Makamu Mwenyekiti wa (CCM) Bara Ndg.Abdulrahman Kinana akizungumza na Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jimbo la Hai katika Mkutano wa Uwasilishaji wa Taarifa ya Utekelezaji wa Ilani ya CCM,Ulioandaliwa na Mbunge wa Jimbo Hilo Ndg.Saashisha Mafuwe .(Picha na Fahadi Siraji)

Na: MWANDISHI WETU

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Abdulrahman Kinana, ameziagiza Kamati za Siasa za CCM za wilaya na mikoa kuwafuatilia na kuwachukulia hatua wanachama walioanza kupitapita kusaka uongozi hususani ubunge na udiwani na uenyekiti wa serikali za mitaa.

Amesema wanaofanya hivyo wanakiuka utaratibu ukiwamo wa sheria na kanuni za uchaguzi za CCM na kweamba watakaobainika muda ukifika hawatapitishwa kugombea nafasi hizo hata kama walipigiwa kura na mkutamo mzima wa Chama. 

Kinana ameyasema hayo jana, wilayani Hai Mkoa wa Kilimanjaro katika mkutano mkuu wa jimbo la Hai kueleza utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020-2025.

“Chama chetu kina utaratibu mzuri sana, tuna vitu vine vinavyoongoza katika uchaguzi wa CCM, cha kwanza Katiba ya CCM, cha pili kanuni za uchaguzi ZA Chama, cha tatu kanuni ya uchaguzi katika vyombo vya serikali kwa wana CCM wanaotaka kugombea katika vyombo serikali kuanzia ubunge, udiwani, uenyekiti wa mtaa au kitongoji.

“Kanuni ya nne ni ya maadili ya Chama. kanuni zote hizi zinasimamia uchaguzi ndani ya CCM na ndani ya serikali, huruhudiwi kutafuta uongozi ndani ya CCM na ndani ya serikali wakati waliochaguliwa wapo na wanafanya kazi mtu yeyote anayetafuta uongozi wakati huu anavunja kanuni hizo nne.

“Nataka nitumie fursa hii kuziagiza kamati za siasa za CCM nchi nzima zikisaidiwa na kamati za maadili nchi nzima kuwafuatilia wale ambao wameanza kuzungukazungaka kutafuta ubunge, udiwani, uenyekiti wa mtaa au kitongoji kuanzi sasa,” alisema.

Alisema iwapo watu hao wameonywa nab ado hawasikii kamati za maadili na kamati za siasa wilaya na mkoa ziwachukulie hatua kwa kadri inavyotakiwa na kanuni za maadili ya uchaguzi ndani ya vyombo vya serikali.

“Hatuna nafasi ya kuhangaishwa na watu wanaotafuta uongozi kipindi hiki, wasubiri hadi mwezi wa saba mwaka 2025, Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) itaamua tarehe ya kwenda kuchukua fomu, kabla ya hapo unavunja kanuni. Na asifikiri mwana CCM yeyote kwamba akianza kampeni kabla akaja kwenye mkutano kama huu akapigiwa kura akawa wa kwanza lakini alianza kampeni, alitoa rushwa, alikivuruga Chama hata upate kura za wajumbe wote hutapita.

“Kwa sababu ili uteuliwe kuna vigezo vingi sana vinatazamwa, kura ulizopata ni moja, lakini je ulizingatia maadili, ulitoa rushwa, je ulizingatia kanuni, je uliwachafua viongozi wenzako walioko madarakani…kwa hiyo unaweza ukawa wa kwanza lakini ukawa wa mwisho.

Awali akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM, Mbunge wa Hai Saasisha Mafuwe, alisema kwa kipindi cha miaka miwili tangu ilipoanza kutekelezwa ilani hiyo, mafanikio mbalimbali yamefikiwa.

Alisema kuwa miongoni mwa utekelezaji huo umegusa sekta ya elimu hususani ujenzi wa madarasa, sekta ya afya, miundombinu na kupeleka huduma ya maji safi kwa wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here