Home BUSINESS DKT. BITEKO AKABIDHI OFISI YA WIZARA YA MADINI KWA MAVUND

DKT. BITEKO AKABIDHI OFISI YA WIZARA YA MADINI KWA MAVUND

#Mhe. Mavunde aainishiwa Vipaumbele vya Wizara ya Madini 2023/24

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko amemkabidhi Ofisi ya Wizara ya Madini kwa Mhe.Anthony Mavunde ili aanze rasmi kazi ya kuiongoza Wizara hiyo.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo Septemba 4, 2023 katika Ofisi za Wizara ya Madini jijini Dodoma ambapo Dkt. Biteko ametumia fursa hiyo kumkabidhi Waziri Mavunde vipaumbele vya Wizara ya Madini kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024.

Vipaumbele alivywasilisha Dkt.Biteko ni pamoja na Kuimarisha Ukusanyaji wa Maduhuli na kuongeza mchango wa Sekta ya Madini kwenye Pato la Taifa, kuendeleza madini Muhimu na madini Mkakati, kuhamasisha shughuli za uongezaji thamani madini na kuhamasisha uwekezaji na biashara katika Sekta ya Madini.

Vipaumbele vingine ni Uanzishwaji wa Minada na Maonesho ya madini ya vito, Kuwaendeleza na kusogeza huduma za ugani kwa wachimbaji wadogo na kuzijengea uwezo taasisi zilizo chini ya Wizara ya Madini ili ziweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Dkt. Biteko ametumia fursa hiyo kuwashukuru viongozi na Watumishi wa Wizara ya Madini na Taasisi zake kwa ushirikiano mkubwa waliomuonesha katika kipindi chake cha utekelezaji wa majukumu mbalimbali.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesisitiza kuwa ataonesha ushirikiano kwa watumishi wa Wizara ili kufikia malengo yaliyowekwa kwa Mwaka wa Fedha 2023/24.

Naye, Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amemshukuru Dkt. Biteko kwa ushirikiano aliompatia katika kipindi walichofanya kazi pamoja na kumtakia Kheri katika majukumu yake mapya.

Akizungumza kwa niaba ya watumishi wote Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula amemuhakikishia Waziri Biteko kuwa watumishi watampatia ushirikiano wa kutosha Waziri Mavunde katika kutekeleza majukumu yake.

Viongozi wengine walioshiriki katika Makabidhiano hayo ni Katibu Mkuu Wizara ya Madini Kheri Mahimbali, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya madini na Watumishi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here