Home BUSINESS BASHE ATAKA WATANZANIA KUTUMIA AGRF KULETA TIJA KWENYE KILIMO

BASHE ATAKA WATANZANIA KUTUMIA AGRF KULETA TIJA KWENYE KILIMO

Waziri wa Kilimo Mhe. Husein Bashe akizungumza kwenye mahojiano na waandishi wa habari mara baada ya kumalizika kwa kikao cha mawaziri kilichofanyika leo Septemba 5,203 kwenye Mkutano wa Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika unaoendelea Jijini Dar es Salaam.

 DAR ES SALAAM

Waziri wa Kilimo Mhe. Husein Bashe amewataka Watanzania kuutumia mkutano wa Mifumo ya Chakula (AGRF) unaoendelea Jijini Dar es Salaam, katika kuleta tija kwenye Sekta ya kilimo, kwa kupata mbegu bora na mbolea kwa wakati na kwa gharama nafuu.

Waziri Bashe ameyasema hayo leo Septemba 5,2023 kwenye mahojiano na waandishi wa habari katika mkutano huo, na kueleza kuwa lengo la mkutano huo ni kuijulisha Dunia rasilimali zilizopo nchini na namna gani Watanzania watashiriki kuzitumia ili waweze kufanya biashara na mataifa mengine Duniani na hasa biashara ya chakula kwa kuwa Dunia inatarajia kuwa na watu bilioni tisa ifikapo mwaka 2030, ambapo kwa Bara la Afrika inakadiriwa kufikia watu bilioni mbili, na Tanzania watu milioni 80 ambao wote wanahitaji chakula.

“Kufanyika kwa mkutano huu hapa nchini, kutaweza kutatua changamoto mbalimbali  zinazowakabili wakulima  kwa kuwa kilimo kinahitaji fedha, na pia uwekezaji wa kumsaidia  mkulima mdogo ama mkubwa anahitaji mitaji hivyo mkutano huu umewaleta pamoja wawekezaji mbalimbali ambao watawezesha wakulima kwa mitaji” 

“Kwa sasa Tanzania inakabiliwa na  changamoto ya kupanda kwa bei za vyakula, hii inatokana na tija ya uzalishaji wa chakula kwa mkulima mdogo shambani kushuka na gharama za uzalishaji kupanda. Hivyo mkutano huu utaisaidia nchi kwa kuwa wawekezaji wengi wataweka fedha kwa ajilii ya kusaidia wakulima wadogo” amesema.

Amesema Katika mkutano huo Benki ya Dunia itazindua mradi wa Dola milioni 300, kwa ajili ya umwagiliajii huku Benki ya Maendeleo AfriKa (ADB) inatarajiwa kuzindua mradi wa Dola milioni 100 ifikapo mwaka 2024,  kwa ajili ya kuwasaidia vijana katika kilimo.

Aidha ameeleza kuwa pamoja na mambo mengine, Serikali ina mkakati wa kuchimba visima 67,500, matanki ya maji lita 5,000,  hadi 1,200,000 lengo ni kufikisha hekari 8,000,000 za umwagiliajii ifikapo mwaka 2030 ikiwa na lengo la kufanya kilimo cha umwagiliaji kwa mwaka mzima.

Mkutano huo wa siku tatu umeandaliwa na Jukwaa la Mfumo wa Chakula Afrika (Africa Food Systems Forum), linalowaleta Wadau pamoja kujadilii hatua za kuboresha kilimo na mifumo ya chakula barani Afrika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here