Home BUSINESS WAZIRI MKUU MSTAAFU PINDA: TIC TUMIENI BALOZI ZETU NJE YA NCHI KUVUTIA...

WAZIRI MKUU MSTAAFU PINDA: TIC TUMIENI BALOZI ZETU NJE YA NCHI KUVUTIA WAWEKEZAJI

Na. Mwandishi Wetu-MBEYA.

Waziri Mkuu Mstaafu Mhe. Mizengo Kayanza Peter Pinda ametembelea Banda la Kituo Cha Uwekezaji Tanzania (TIC), katika Maonesho ya Nanenane yanayofanyika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya.

Mhe. Pinda ametembelea maonesho hayo leo tarehe 07 Agosti, 2023 akiambatana na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Charles Makongoro Nyerere.

Pamoja na mambo mengine Mhe. Pinda ameeleza kuwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania kinatakiwa kuendelea kutumia balozi zilizopo nje ya nchi katika kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini.

Aidha, Mhe. Pinda amesisitiza kusambaza vipeperushi vinavyoonesha fursa mbalimbali zilizopo nchini sehemu mbalimbali duniani hususan kwenye balozi za Tanzania kwa ajili ya kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini.

Mhe. Pinda aliendelea kueleza “Balozi ziweze kushirikishwa katika kuwapata wawekezaji wazuri na kuepuka wawekezaji kuishia kuangukia mikononi mwa matapeli ambao huwatapeli wawekezaji na kuichafua nchi”.

Mhe. Pinda aliendelea kusisitiza kuwa anapokuwa katika safari za nje ya nchi anakutana na wawekezaji na kuwaelekeza kuwasiliana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania kwani ndiyo taasisi ya serikali yenye jukumu la kusimamia masuala ya uwekezaji Nchini.

Vilevile ameeleza kuwa kuanzia tarehe 5-8 Septemba, 2023 kutakuwa na Maonesho ya Kilimo hivyo watanzania tutumie fursa hii kwa ajili ya kutangaza fursa za uwekezaji katika maeneo ya kilimo.

“TIC iweze kuomba nafasi ya kufanya wasilisho la fursa za uwekezaji kwani zaidi ya wadau 3000 wanatarajia kushiriki” Ameongeza Pinda.

TIC inashiriki maonesho ya Nanenane kwenye mikoa mbalimbali kama, Kitaifa – Mkoani Mbeya, Arusha, Simiyu, Dodoma, Morogoro, Tabora na Lindi.

Kuboreshwa kwa mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na kuimarishwa kwa mahusiano ya kikanda na kimataifa yamekuwa ni chachu ya kuwavutia wawekezaji Nchini.

Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here