Home BUSINESS TUUZE KOROSHO ZILIZOBANGULIWA-MAJALIWA

TUUZE KOROSHO ZILIZOBANGULIWA-MAJALIWA

*Asisitiza korosho ilizobanguliwa zinafaida zaidi ya ghafi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakulima zao la korosho wafanye kilimo cha kibiashara kwa kuacha kuuza korosho ghafi na badala yake wauze zilizobanguliwa ili kujiongeza tija zaidi.

“Wakati wa kubadilika umefika, tutumie fursa hii kujenga viwanda vya kubangulia korosho na kuwawezesha wakulima kubangua na kuuza katika masoko ya nje na ndani.”

Amesema bei ya kilo moja ya korosho iliyobanguliwa ni takribani shilingi 13,000 na ghafi ni takribani shilingi 2,000, ukibangua kilo nne za korosho ghafi unapata kilo moja ya ya korosho iliyobanguliwa.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Agosti 14, 2023) wakati akiongea na wananchi wa halmashauri ya Mji wa Newala akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Mtwara.

Amesema kitendo cha kusafirisha korosho ghafi nje ya nchi kinawakosesha baadhi ya mapato yatokanayo na maganda ya korosho ambayo yanatumika kutengeneza mafuta.

Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wamiliki wa viwanda vya kubangua korosho watoe nafasi kwa wakulima kwenda kubangua korosho zao na kuwatoza gharama za ubanguaji.

“Wenye viwanda igeni mfano wa kiwanda cha kubangua korosho cha Organic Growth Limited (OGL) kilichopo Tandahimba ambacho kinaruhusu wakulima kwenda kubangua.”

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed, kusimamia utekelezaji wa Mkataba wa Usambazaji wa umeme katika wilaya ya Newala unaotekelezwa na kampuni ya Central Electric International.

Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO mkoa wa Mtwara Mhandisi, Tawakal Rwahila Alisema mkandarasi huyo alipaswa kukamilisha kazi hiyo mwezi Apriri 2023.

Mhandisi Rwahila amesema mkandarasi huyo alipewa kazi ya kusambaza umeme katika vijiji 70 vya wilaya ya Newala mwezi Agosti 2021 na amekuwa na utendaji usioridhisha.

Kadhalika, Waziri Mkuu amekukagua maendeleo ya ujenzi wa majengo ya uboreshaji wa utoaji wa huduma za afya katika hospitali ya Mji Newala uliogharimu shilingi milioni 800.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, AGOSTI 14, 2023.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here