Home BUSINESS RAIS MWINYI AIPONGEZA BENKI YA CRDB KWA KUIMARISHA AFYA NCHINI

RAIS MWINYI AIPONGEZA BENKI YA CRDB KWA KUIMARISHA AFYA NCHINI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi ameiopongeza Benki ya CRDB kwa juhudi inazozionyesha kuboresha afya nchini na kuzitaka kampuni nyingine binafsi kujitoa ili kuongeza nguvu kwani mahitaji ni makubwa.


Rais Mwinyi ametoa pongezi hizo kwenye kilele cha CRDB Bank Marathon kilichofanyika leo Agosti 13 katika viwanja vya The Green vilivyopo Oysterbay jijini Dar es Salaam na kuwashuhudia washindi wakiondoka na mamilioni ya zawadi baada ya kuonyesha kasi kubwa kuliko wakimbiza upepo wengine zaidi ya 7,000 waliojitokeza na kushiriki.

 

Akieleza mchango wa CRDB Bank Marathon kwenye sekta ya afya, Rais Mwinyi amesema ni mkubwa na unagusa pande zote za muungano kwa kuwawezesha wasio na uwezo wa kugharimi amatibabu yao pamoja na kuimarisha miundombinu.

“Fedha zinazokusanywa kutoka kwa washiriki wa mbio hizi za hisani zinaelekezwa kwenye matibabu ya Watoto wenye matatizo ya moyo pamoja na wanawake wenye ujauzito hatarishi. Mwaka huu fedha hizi zitajenga kituo cha afya kule Zanzibar, huu ni mchango mkubwa unaowagusa Watanzania wengi. Nawaomba wadau wengine nao waone namna wanavyoweza kushirikiana na serikali kuboresha huduma za afya,” amesema Rais Mwinyi.

 

Hata kuratibu mbio hizi zilizokusanya shilingi bilioni moja zitakazoelekezwa kwa walengwa waliokusudiwa mwaka huu, Rais Mwinyi amesema kulihitaji ushiriki wa watu wenye nia moja na akaipongeza kampuni ya Sanlam Insurance ambayo ndio mdhamini mkuu wa mwaka huu.

“Benki ya CRDB inashirikiana na washirika wake kufanikisha mbio hizi. Niwapongeze kampuni ya Sanlam ambao niliwaona ikulu kule Migombani Zanzibar. Homgereni Sanlam kwa kuwa sehemu ya mchango huu mkubwa kwa jamii,” amepongeza Rais.

 

Akieleza namna mbio za CRDB Bank Marathon zinavyoigusa jamii, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema kwa misimu mitatu iliyotanguliwa, fedha zilizokusanywa kutokana na usajili wa washiriki na zile zilizochangwa na washirika, zimewagusa watu wengi.


“Mwaka 2020 wakati tunaanza, zaidi ya watu 4,000 walishiriki na kufanikisha kukusanya shilingi milioni 200 zilizofanikisha upasuaji wa moyo kwa watoto 100 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), pamoja na programu ya utunzaji mazingira ya pendezesha Tanzania,” alsema. 

 

Aliongeza kuwa mwaka 2021 kulikuwa na washiriki 5,000 na jumla ya shilingi milioni 350 zilikusanywa ambazo zilitumika katika upasuaji wa moyo kwa watoto wengine 100 na kujenga Kituo cha Mawasiliano Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.


Alifafanua kuwa mwaka jana, jumla ya shilingi milioni 470 zilikusanywa kutoka kwa washiriki 6,000 ambazo zilitumika katika gharama za matibabu ya  wagonjwa watoto 100 JKCI na wanawake wenye ujauzito hatarishi na walio na maradhi ya fistula katika Hospitali ya CCBRT. 

 

Kutokana na mafanikio hayo, Nsekela amesema msimu huu wa nne wa CRDB Bank Marathon una malengo makuu manne ambayo ni kujenga kituo cha afya ya mama na mtoto visiwani Zanzibar, kuchangia matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo, kuchangia matibabu ya wanawake wenye ujauzito hatarishi na wanaougua fistula pamoja na kuendelea programu ya pendezesha Tanzania kwa kuimarisha bustani za Zanzibar ikiwamo Bustani ya Jamhuri, Bustani ya Migombani-Botanic Garden, Bustani ya Tenga-Mnazi Mmoja, Bustani ya Mbele ya Ikulu Migombani pamoja na Njia Nne za Michenzani.

Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB Bank Foundation, Martin Warioba alisema mafanikio ya mbio wanazoziratibu waliyoyapata ndani ya miaka mitatu iliyopita yamevuka mipaka kwani katika mwaka wa pili tu zilitambulika kimataifa na Chama cha Usajili na Upimaji wa Mbio za Kimataifa (AIMS) na Shirikisho la Kimataifa la Mchezo wa Riadha (World Athletics).

“Hii si tu imekuwa ni heshima kwa Benki yetu lakini pia ni heshima kwa nchi yetu. Kwa utambulisho huu wa kimataifa, mbio za CRDB Bank Marathon zinavutia wakimbiaji kutoka mataifa mbalimbali ulimwenguni hivvo kuzifanya kuwa sehemu ya kutangaza utalii wa nchi yetu,” alisema Warioba.

Warioba alisema kuwa mafanikio ya mbio za mwaka huu yamechangiwa na wadau kadhaa wanaoshirikiana na Benki ya CRDB ambao ni kampuni ya Sanlam Insurance, Alliance Life Insurance, Clouds Media Group Jubilee Allianz & Life Insurance, Heritage Insurance, Britam Insurance, Strategis Insurance, A1 Outdoor, Gardaworld, Mwananchi Communications, IPP Media, Sahara Media, Softnet, BEVCO, Hyatt Regency, na Spik & Span.

Afrika Mashariki wagawana zawadi
Zawadi zenye thamani ya zaidi ya shilingi 100 zilizotolewa kwa washindi wote walioshiriki kilomita 42, kilomita 21, kilomita 10 na kilomita tano pamoja na kilomita 65 kwa waendesha baiskeli zilikwenda kwa wawakilishi kutoka karibu mataifa yote ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Kwenye kilomita 42 (full marathon), Jakline Juma wa Tanzania na Moses Menginch wa Kenya waliongoza makundi yao hivyo kuondoka shilingi milioni 10 walizoshinda huku nafasi ya pili ikienda kwa Paskalia Chipkorir wa Kenya na Jonathan Akankwasa walizawadiwa shilingi milioni 5 na Nancy Cheptegei wa Uganda na Rashid Muna wakiondoka na shilingi milioni 2, baada ya kushika nafasi ya tatu.

Kwenye mbio za kilomita 21 (nusu marathon), Watanzania waling’ara katika makundi yote mawili, yaani wanawake na wanaume baada ya Magdalena Crispin na Josephat Joshua kuongoza. Nafasi ya pili ilikwenda kwa Atalena Napule Gasper wa Sudan na Nangat Willy wa Kenya huku nafasi ya tatu ikikamatwa na Failuna Matanga wa Tanzania na Panuel Mkingo wa Kenya.

Ceclia Panga, Transfora Musa na Neema Kisuda waliwaongoza wanawake kukimbia kilomita 10 huku Shuemery Mohamed, Josephat Tiophil na Jonas John wakifanya hivyo kwa wanaume. John Msigwa, Danidi Kisoni na Justine Mbegu walikuwa moto wa kuotea mbali kwa wavulana waliokimbia kilomita tano.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi akimvalisha medali ya kushiriki mbio za hisani za CRDB Bank Marathon Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela. Wengine kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Alliance LifeA ssurance, Byford Mutimusakwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya akurugenzi wa Benki ya CRDB, Neema Mori. Kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB Bank Foundation, Martin Warioba, Waziri wa Habari, Vijana na Michezo Zanzibar, Tabia Mwita, Waziri wa Utamaduni,

Sanaa na Michezo, Balozi Dkt Pindi Hazara Chana na Mke wa Rais Mwinyi,
Mama Mariam  Mwinyi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here