Na:Neema Adriano
TGNP kushirikiana na PELUM Tanzania kwa udhamini wa SeedChange na Global Affairs Canada wameweza kuonesha kazi inayofanywa na wanawake wa vijijini, ambao ni waleta mabadiliko ikiwemo mbegu za mazao mbalimbali walizozigundua.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 7,2023, Afisa Programu Sera,Uchechemuzi na Ujenzi wa Nguvu za pamoja, Rugathe Loakaki wakati wa maonesho hayo yaliyofanyika katika Viwanja vya Nanenane Morogoro,amesema kuwa ameona muitikio mzuri sana kutoka kwa washiriki na wadau mbalimbali na katika kilimo ikolojia lakini pia katika agenda zao za kupinga ukatili wa kingono.
Amesema pia wanahamasisha ushiriki wa wanawake katika uongozi hayo ni matarajio mazuri ambayo wataendelea kushiriki katika maonesho ya namna hii na kupitia ushiriki huo wananchi wameweza kujifunza mambo kadha wa kadha katika maeneo ambayo ameyataja kulingana na muitikio huo ambao ameuona.
“Watakapokwenda kutumia hii Elimu ambayo wameipata hakika tutaweza kufikia adhma yetu kuwa Nchi ya kwanza kuwa ghala la chakula la Taifa,Afrika na hata Dunia lakini pia tutaweza kuiona Kauli mbiu yetu ya nanenane mwaka huu,ikienda kuishi ambapo ni Vijana na Wanawake ni Msingi Imara wa mfumo endelevu wa Chakula,” amesema Bi.Loakaki.
TGNP na Mtandao wameshiriki katika maonesho hayo na walitembelewa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Selemani Jafo,Mkuu wa Wilaya ya Korogwe,Jokate Mwegelo na wengineo.