Home LOCAL MSD YATAKIWA KUONGEZA KASI YA USAMBAZAJI WA BIDHAA ZA DAWA

MSD YATAKIWA KUONGEZA KASI YA USAMBAZAJI WA BIDHAA ZA DAWA

Na WAF, Dodoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI imeitaka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) nchini kuongeza kasi ya usambazaji wa bidhaa za Dawa pamoja na kuwa na maghala ya dawa katika kila Halmashauri.

Wito huo umetolewa leo Mwenyekiti wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI, Mhe. Stanslaus Nyongo baada ya kupokea taarifa ya usambazaji wa bidhaa za Afya kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Bw. Mavere Tukai katika kikao cha Kamati kilichofanyika Bungeni Jijini Dodoma.

“Kwanza naipongeza sana Wizara kwa hatua mnazoendelea kuchukua za kuhakikisha upatikanaji wa bidhaa za Dawa na vifaa tiba inaongezeka lakini pia niwatake muongeze jitihada hizo kwakuwa uhitaji wa bidhaa hizo ni mkubwa nchini”, ameeleza Mhe. Nyongo

Kwa upande wake Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu wakati akijibu maswali ya Wajumbe wa kamati hiyo amesema Serikali imewapa mtaji Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili kuhakikisha Dawa na vifaa tiba zinapatikana kwa wakati na kusambazwa nchini.

“Tumepokea mapendekezo yote ya kamati, Serikali tutahakikisha tunaiwezesha MSD ili kutekeleza majukumu yake ipasavyo pamoja na kuwafutia madeni waliyonayo”, amesema Waziri Ummy

Pia, Waziri Ummy ameitaka MSD kujipima katika upatikanaji wa Dawa, Vifaa tiba pamoja na vitendanishi kwenye huduma za Afya ngazi ya msingi.

Nae, Mkurugenzi Mkuu wa Bohari ya Dawa (MSD) Bw. Mavere Tukai wakati akiwasilisha taarifa yake kwa kamati hiyo amesema usambazaji wa bidhaa za afya kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kupitia Mfumo wa Ugavi Shirikishi umefanikiwa kwa asilimia 97.

Pia, amesema kwa Mwaka wa fedha 2022/23, Bohari ya Dawa ilianza usambazaji wa bidhaa za afya mara Sita kwa mwaka badala ya mara Nne kama ilivyokuwa awali.

“Lengo la usambazaji huu ni kupunguzia vituo vya kutolea huduma za afya muda wa kusubiri bidhaa hivyo kuimarisha upatikanaji wa bidhaa za Afya nchini”, ameeleza Bw. Mavere

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here