Home BUSINESS MBIBO AWAOMBA MABALOZI KUISAIDIA WIZARA KUTIMIZA NDOTO ZA WAASISI SEKTA YA MADINI

MBIBO AWAOMBA MABALOZI KUISAIDIA WIZARA KUTIMIZA NDOTO ZA WAASISI SEKTA YA MADINI

Kamishna wa Madini awaeleza kuweka Msukumo kwenye Madini Mkakati

Dodoma

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Msafiri Mbibo amewaomba Mabalozi Wapya walioteuliwa hivi karibuni kuiwezesha Sekta ya Madini kutimiza Ndoto za Waasisi wa Taifa kwa kuendeleza jitihada za Wizara za kuhakikisha rasilimali madini zinatumika kujenga uchumi imara, maendeleo ya nchi na watu.

Ili kutimiza ndoto hizo, Mbibo amewaomba kutangaza fursa za uwekezaji zilizopo kwenye Sekta ya Madini na kuvutia uwekezaji nchini kwa lengo la kuongeza mchango wake kiuchumi na kimaendeleo.

Mbibo ameyasema hayo Agosti 30, 2023 jijini Dodoma katika kikao kilicholenga kuwajengea uwezo kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo katika sekta ya Madini ikiwemo maeneo muhimu ya kipaumbele na yanayopaswa kupewa msukumo kiuwekezaji ikiwemo kuimarisha na kujenga ushirikiano na nchi wanazokwenda.

Mabalozi waliotembelea wizara ya madini ni Balozi Joseph Sokoine anayekwenda nchi ya Canada, Balozi Fatma Rajabu anayekwenda nchini Oman, Balozi Naimi Aziz anayekwenda nchini Austria, Balozi Ally Mwandini anayekwenda nchini Ufaransa na Balozi Ciaser Waitara anayekwenda nchini Namibia.

Aidha, amewaomba Mabalozi hao kuisaidia wizara kupata maarifa mapya ya namna bora ya kuiendeleza Sekta ya Madini kupitia uzoefu watakaoupata katika nchi hizo.

Akizungumza katika kikao hicho kwa niaba ya mabalozi hao, Balozi Joseph Sokoine amesema mabalozi hao waliona upo umuhimu wa kukutana na wadau muhimu ili kupata taarifa za kina na muhimu zitakazowasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao katika vituo vyao vya kazi.

‘’ Tunashukuru sana kwa darasa hili, huu ni mwanzo na tutaendelea kushirikiana, msisite kuwasiliana na sisi kwa chochote milango yetu iko wazi kwa manufaa ya kukuza uchumi wa taifa letu,’’ amesema Balozi Sokoine.

Wakichangia mada kwa nyakati tofauti, wameishauri wizara kuendelea kujitangaza katika mataifa mbalimbali kutokana na umuhimu wa Sekta ya Madini kiuchumi pamoja na kuhakikisha balozi mbalimbali zinawezeshwa kwa taarifa muhimu zinazohusu masuala ya uwekezaji katika Sekta ya Madini.

Naye, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga akizungumza katika kikao hicho, amewaeleza mabalozi hao kuhusu kipaumbele cha wizara kiuwekezaji kuwa ni kuendeleza madini mkakati kutokana na mahitaji makubwa ya madini hayo duniani na kuyataja baadhi ya maeneo ambayo yanahitaji uwekezaji kuwa ni katika utafiti na uchimbaji wa madini hayo.

Katika kikao hicho, taasisi zilizochini ya wizara zimepata wasaa wa kutoa mawasilisho ya taarifa muhimu za kisekta zenye lengo la kuhamasisha na kuvutia uwekezaji.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here