Home BUSINESS MAONESHO YA MADINI YAUFUNGUA MKOA WA LINDI

MAONESHO YA MADINI YAUFUNGUA MKOA WA LINDI

Ruangwa – Lindi.
 
Maonesho ya Kwanza ya Madini na Fursa za Uwekezaji yanayoendelea Mkoani Lindi yametajwa kuufungua mkoa huo kiuchumi na kuongeza fursa mbalimbali za uwekezaji katika Sekta ya Madini.Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko Agosti 25, 2023 Mkoani Lindi alipotembelea maonesho hayo na kuzungumza na wadau wa Sekta ya Madini wanaoshiriki maonesho hayo.

Dkt. Biteko amesema, maonesho yamewakutanisha wadau mbalimbali wa Sekta ya Madini kutoka nchi zaidi ya 10 waliofika kujifunza na kuangalia fursa za uwekezaji katika mkoa huo.

Mbali na Tanzania  wageni wengine walioshiriki wametoka katika Nchi ya China, Marekani, Canada, Australia, Japan, Srilanka na Finland.

“Naomba kutoa wito kwa wananchi wa Lindi kutoa ushirikiano kwa wawekezaji  wanaofika kuwekeza nchini ili kwa pamoja tunufaike na uchimbaji wa rasilimali madini,”amesema Dkt. Biteko.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesisitiza kuwa shughuli na biashara katika Sekta ya Madini zifanywe na Watanzania wenye sifa ili wazawa wanufaike na  uchumi wa madini na hatimaye kuongeza mchango wa Sekta katika  Pato la Taifa.

Naye, Meneja wa Huduma ya Jiolojia kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Solomon Maswi akitoa wasilisho katika Maonesho ya Kwanza ya Madini na Fursa za Uwekezaji Wilayani Ruangwa Mkoa wa Lindi. Maswi amesema GST imechora ramani ya Jiolojia ya Mkoa wa Lindi na nchi nzima kuonesha fursa mbalimbali zilizopo kuanzia ngazi ya mkoa na nchi nzima ambayo inapatikana kwa lugha ya Kiswahili.

Aidha, Maswi amesema kuwa GST imefanya Utafiti wa awali na kuja na mapendekezo ya Madini Mkakati 31 na Madini Muhimu 11 kwa nchi nzima ambapo Mkoa wa Lindi una Madini Mkakati sita ambayo ni Chuma, Kinywe, Dhahabu, Shaba, Magnesite, Shaba pamoja na Madini Muhimu manne ambayo ni Jasi, Chokaa, Chumvi na Chuma.

Vile vile, Mtendaji Mkuu wa Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) Dkt. Venance Mwasse amesema, shirika hilo limetelekeza majukumu mbalimbali hususan katika ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kusafisha chumvi ili kupata soko la uhakika mkoani Lindi.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Lindi Mhandisi Iddi Msikozi amesema lengo la maonesho ya Madini Lindi ni kuonesha dunia kwamba Tanzania kuwa imebarikiwa kuwa rasilimali Madini za kutosha na wadau wamekaribishwa kuwekeza katika mkoa huo ili Watanzania wanufaike na uchumi wa madini.

Wengine waliotoa mada katika maonesho ni pamoja na Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi Hassan Ngoma,  Mjiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Japhet Fungo, Mjiolojia kutoka Chuo Kikuu cha Yunnan Prof. Xuance Wang na Katibu Mkuu Umoja wa Wachimbaji wa Madini  (UVIWAMA) Castory Mtonga

  

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here