Home BUSINESS  GST KUSHIRIKIANA NA STAMICO KUCHUNGUZA UBORA WA SAMPULI

 GST KUSHIRIKIANA NA STAMICO KUCHUNGUZA UBORA WA SAMPULI

Naibu Waziri wa Madini Dkt. Steven Kiruswa amepokea taarifa kuhusu mpango wa Mgodi wa Kiwira-Kabulo unaomilikiwa na Shiriki la Madini la Taifa (STAMICO) kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 ni kuzalisha Makaa ya Mawe yenye thamani ya shilling bilioni 40.

Dkt. Kiruswa amepokea taarifa hiyo kutoka kwa Mratibu wa Mgodi wa Kiwira-Kabulo Mhandisi Peter Maha wakati akiwasilisha taarifa ya mafanikio, changamoto na mipango ya Mgodi katika Mwaka wa Fedha 2023/24.

Ili kutekeleza hilo, Dkt. Kiruswa ameiagiza Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) kushirikiana na STAMICO katika uchungizi wa sampuli za Maabara hususan katika kuchunguza ubora wa Makaa ya Mawe.

Ametoa maagizo hayo baada ya kutembelea mgodi wa Kiwira-Kabulo uliopo katika Kijiji cha Kapeta Kata ya Ikinga wilayani Ileje mkoa wa Songwe ambapo amesema GST tayari ina Ithibati inayotambulika Kimataifa hivyo Taasisi hizo mbili zishirikiane kupima ubora wa Makaa hayo mgodini hapo ili kupunguza asumbufu kwa wateja wanaotaka kupata vipimo kutoka Maabara zilizo thibitishwa Kimataifa.

Aidha, Dkt. Kiruswa amesema, kutokana na uwekezaji mkubwa uliofanyika katika mgodi wa Kiwira-Kabulo, ni vyema akatafutwa mwekezaji mkubwa Ili ashirikiane na STAMICO katika uchimbaji wa makaa ya mawe ambapo kwa sasa yanahitajika kwa wingi katika nchi mbambali duniani ili kuongeza uzalishaji na kuchimba kwa faida kwa lengo la kunufaisha uchumi wa nchi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Kiruswa ameipongeza STAMICO kwa kuendelea kufanya vizuri katika uzalishaji wa makaa ya mawe na kuendelea kuchangia huduma kwa jamii zinazozunguka mgodi kama Sheria zinavyoelekeza na pia, amewasihi watumishi wote kuendelea kufanya kazi kwa bidii na kujitoa ili kuandika historia mpya kati ya miradi ya STAMICO iliyofanikiwa.

Pia, Dkt. Kiruswa ameahidi kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazoukabili mgodi huo ikiwemo upungufu wa wafanyakazi, upungufu wa vitendeakazi, madai ya watumishi na uchakavu wa majengo.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mgodi wa Kiwira-Kabulo Mhandisi Peter Maha amemshukuru Naibu Waziri kwa kufanya ziara katika mgodi huo ambapo amesema kitendo hicho kitaongeza morali ya kazi na kuchochea maendeleo ya uzalishaji katika mradi huo ambao kwa kiasi kikubwa umefanikiwa kuendeleza uzalishaji wa makaa ya mawe na kuhudumia soko la ndani na nje ya nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here