Home BUSINESS DKT. BITEKO ATOA WITO WACHIMBAJI KUTUMIA BANDARI YA MTWARA KUSAFIRISHA MAKAA YA...

DKT. BITEKO ATOA WITO WACHIMBAJI KUTUMIA BANDARI YA MTWARA KUSAFIRISHA MAKAA YA MAWE

  #Ruvuma Coal yapewa Kongole na Dkt. Biteko

Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amewataka Wachimbaji wa Makaa ya mawe na wadau wenye wateja wa makaa hayo kutoka nje ya nchi kuitumia Bandari ya Mkoani Mtwara ili kusafirisha bidhaa katika bandari hiyo.

Dkt. Biteko ametoa wito huo Agosti 24, 2023 alipotembelea na kuzungumza na uongozi wa bandari ya Mtwara ili kujionea shughuli zinazofanywa hususan katika usafirishaji wa makaa ya mawe kwenda nje ya nchi.

Amesema kuwa, miundombinu katika bandari ya Mtwara inaendelea kuboreshwa ili kuhakikisha makaa ya mawe yanafika kwa wakati nje ya nchi yalipo masoko ya uhakika ya bidhaa hiyo.

“Nawapongeza sana kwa kutengeneza mazingira mazuri angalau wanajitahidi sana kuhakikisha makaa ya mawe yanayofika hapa yanajazwa kwenye meli na kusafirisha nje ya nchi,” amesema Biteko

Dkt. Biteko ameongeza kuwa, biashara ya makaa ya mawe imekuwa kubwa hivi karibuni kutokana na uhitaji wa makaa hayo duniani na hivyo bandari ya Mtwara kufanya shughuli nyingi za usafirishaji wa makaa nje ya nchi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) imekuwa msaada mkubwa katika usafirishaji wa bidhaa zinazotokana na Sekta ya Madini kwenda kwenye masoko ya nje kwa urahisi zaidi.

Pia, ameipongeza Kampuni ya Ruvuma Coal inayochimba makaa ya mawe kwa kuagiza mtambo ambao utakua mkanda wa kusafirisha makaa moja kwa moja hadi kwenye meli kwa kushirikiana na Mamlaka ya bandari.

“Mitambo hii itatusaidia sana kupunguza muda wa kujaza wa mizigo kwenye meli utakua mfupi zaidi kuliko hivi sasa,” amesema Dkt. Biteko.

Kwa upande wake, Afisa Madini Mkazi Mkoa wa Mtwara Mhandisi Ephraim Mushi amesema, bandari ya Mtwara imepokea meli zinazofika kupakia makaa ya mawe kwenda nje ya nchi hususan nchi ya India, Senegal, France, Egypt, Poland, Ghana, Kenya, Congo na China.

Aidha, Ofisi ya Afisa Madini Mtwara imekuwa na jukumu la utoaji wa vibali ( Export Permit) na kusimamia upakiaji wa makaa ya mawe kwa kushirikiana na taasisi zingine.

Madini mengine yanayopatikana mkoani Mtwara ni kama vile madini ya ujenzi, dhahabu, shaba, chokaa, udongo mwekundu, chuma, chumvi, Kinywe na Madini Mazito ya Mchanga ( Heavy Mineral Sand).

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here