Zoezi la upokeaji Filamu zitakazo shiriki katika Tamasha la Tuzo za Filamu Tanzania 2023 limeanza rasmi tarehe 11 Agosti 2023 na litadumu kwa wiki 6 hadi tarehe 25 Septemba 2023 ambapo Filamu zitapokelewa kwa njia Tatu ikiwemo, kuwasilishwa Ofisi za Bodi, Kwa njia ya Mtandao – https://taffa.info (mfumo utafunguka tar 17 Aug), pamoja na kuzifuata (Filamu) Mikoani katika mikoa 26 Tanzania Bara.
Filamu zitakazo pokelewa zitahakikiwa na Majaji na zitakazopita katika Mchujo wa kwanza zitapata nafasi ya kuoneshwa kwa hadhira ili kupigiwa kura kupitia kituo cha Azam TV Chaneli ya Sinema Zetu (103), pamoja na vituo vingine vitakavyopenda kuonesha kazi hizo. Kura zitapigwa kwa njia mbili: njia ya ujumbe mfupi wa maneno (SMS), na kupitia mfumo wa kidijiti (https://taffa.info). Aidha, maelekezo mengine ya namna ya kupiga kura yataendelea kutolewa baada ya Mchujo wa kwanza kupitia mitandano ya kijamii ya Bodi ya Filamu.
Pamoja na mambo mengine, Tamasha la Tuzo za Filamu Tanzania 2023 limeongeza wigo wa ushiriki wa Filamu kutoka Nchi za Afrika Mashariki ambazo zimeandaliwa kwa lugha ya Kiswahili ili kuendelea kuithamini na kuikuza lugha hiyo ambayo ni moja ya nembo ya Taifa letu.