Home BUSINESS BRELA YAWANOA WAUZAJI WA MAZAO YA KILIMO NJE NCHI

BRELA YAWANOA WAUZAJI WA MAZAO YA KILIMO NJE NCHI

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Bw. Ramadhani akifungua mafunzo maalum kwa wauzaji wa mazao ya kilimo nje ya nchi mkoani Arusha tarehe 24 Agosti, 2023.

Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Kampuni kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Isdor Nkindi tarehe 24 Agosti, 2023 akiwasilisha mada kuhusu Usajili wa Kampuni na Huduma baada ya Usajili huo, kwenye mafunzo yanayotolewa na Taasisi hiyo Jijini Arusha kwa wauzaji wa mazao ya kilimo nje ya nchi.

Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Majina ya Biashara kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Bw. Harvey Kombe, tarehe 24 Agosti, 2023 akiwasilisha mada kuhusu Usajili wa Majina ya Biashara kwenye mafunzo yanayotolewa na Taasisi hiyo Jijini Arusha kwa wauzaji wa mazao ya kilimo nje ya nchi.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Bw. Ramadhani Madeleka (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo yanayotolewa na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), mkoani Arusha, kwa wauzaji wa mazao ya kilimo nje ya nchi, tarehe 24 Agosti, 2023.

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) tarehe 24 Agosti, 2023 imetoa mafunzo maalum kwa wauzaji wa mazao ya kilimo nje ya nchi mkoani Arusha yenye lengo la kuwajengea uwezo ili kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu urasimishaji biashara.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Arusha, Bw. Ramadhani Madeleka ameeleza kuwa wafanyabiashara wanatakiwa kutumia fursa hii ya kipekee iliyotolewa na serikali kuhakikisha changamoto zao zinatatuliwa.

“Mafunzo haya ni matokeo ya changamoto ambazo mlimueleza Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji katika Jiji la Arusha, hivyo Mheshimiwa Waziri alitoa maelekezo kwa ofisi ya RAS na BRELA kufanya mafunzo wezeshi kwenu ili kuzimaliza changamoto hizo. Tumieni fursa hii vizuri”, ameeleza Bw. Madeleka.

Bw. Madeleka ameipongeza BRELA kwa kuwa chachu ya uanzishwaji, urasimishaji, na uboreshaji wa biashara hapa nchini ikiwa ni pamoja na kuwa kielelezo katika utekelezaji wa uboreshaji wa mazingira wezeshi ya ufanyaji Biashara hapa nchini.

Naye Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Isdor Nkindi ambaye ni Kaimu Mkuu wa Sehemu ya Kampuni, ameeleza kuwa dhima kuu ya mafunzo haya ni kuwawezesha wafanyabiashara kufanya biashara kwa kukidhi matakwa ya sheria.

“Kundi hili ni miongoni mwa makundi mengi ya wafanyabiashara ambayo yatafikiwa na BRELA. Lengo kuu ni kuwasaidia wafanyabiashara wanaouza mazao ya kilimo nje ya nchi kujirasimisha kwa kuwa na Usajili wa Jina la Bishara au Kampuni, kuwa na nembo katika bidhaa zao ambazo zimesajiliwa na kuwa na Leseni za Biashara kundi “A” hatua itakayowawezesha kufanya biashara bila kukwama sehemu yeyote”, ameeleza Bw. Nkindi.

Katika mafunzo hayo ya siku tatu mbali na kutoa elimu pia huduma ya Usajili wa papo kwa papo itatolewa kwa wafanyabiashara wote ambao wamekidhi vigezo.

Akizungumza kwa niaba ya washiriki wa mafunzo hayo Bi. Agness Mushi amesema mafunzo hayo yamemsaidia kutambua urahisi wa kurasimisha biashara tofauti na awali.

“Awali nilikua naogopa kuomba Leseni ya Biashara kundi “A”, Jina la Biashara au Kampuni kwa kuhofia kubanwa na sheria pamoja na gharama, mafunzo haya yamenifanya nione sheria hizi ni rafiki na gharama za Usajili sio kubwa”, amesema Bi. Mushi.

Mafunzo hayo yanafanyika ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Serikali yaliyotolewa tarehe 1 Agosti, 2023 na Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Ashatu Kijaji alipokua ziarani mkoani humo. Mafunzo kama hayo yatafanyika pia mkoani Kilimanjaro kuanzia tarehe 28 hadi 30 Agosti 2023.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here