Amesema hayo, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na wafanyabiashara wa dawa na vifaa tiba akiwa katika Jiji la Hyderabad nchini India kwenye mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Wazalishaji na wauzaji wa dawa nchini India (Pharmaceuticals Export Promition Council of India) ukiwa na lengo kusikiliza hoja mbalimbaki za wafanyabiashara pamoja na kutoa ufafanuzi katika maeneo mbalimbali yatayosaidia kuboresha mazingira ya biashara hiyo.
Katika kikao hicho, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwa kushirikiana na Wataalamu kutoka TMDA na MSD walitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizoulizwa na wafanyabiashara ambao walitaka kupata uzoefu wa namna huduma za dawa zinavyofanyika nchini Tanzania.
“Serikali kupitia Mamlaka ya Dawa na Vifaa tiba (TMDA) imeweka utaratibu wa wazi kwa kila mteja anayefika kupata huduma au kufanya biashara”amesema Waziri Ummy.
Pia, ametoa wito kwa wafanyabiashara hao kutoa ushirikiano mkubwa pindi wanapotakiwa kuzingatia taratibu za ukaguzi, usajili na uingizaji wa dawa na vifaa tiba nchini Tanzania ili kuepuka changamoto mbalimbali zinazoweza kuzuilika.
Sambamba na hilo, amewataka wafanyabiashara hao kutumia fursa zilizopo Tanzania hususan, uanachama wa jumuiya za EAC na SADC zenye watu wapatao Milioni 745.1 ambalo ni soko kubwa kwa biashara ikiwemo biashara ya dawa na vifaa tiba.
Waziri Ummy amewakaribisha wafanyabiashara wa India kuja nchini Tanzania kufanya biashara na uwekezaji katika viwanda vya kuzalisha daw ana vifaa tiba ili kuunga mkono ajenda kubwa ya maendeleo ya viwanda ya Tanzania.
Aidha, alieleza kuwa, kwa kiasi kikubwa Serikali ya Rais Dkt. Samia imeboresha mazingira ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini kupitia utekelezaji wa Mwongozo wa Taifa wa Uwekezaji ikiwa ni pamoja na Serikali kufanyia kazi changamoto mbalimbali zilizokuwepo kwa wawekezaji na wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.