Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia kahawa, wakati alipo tembelea banda la Tanganyika Instant Coffee katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara, yanayofanyika kwenye Viwanja vya Maonesho ya Sabasaba, jijini Dar es Salaam. Julai 05, 2023. Kulia ni Meneja Masoko wa Kampuni hiyo Rewina Peter. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akioneshwa ramani ya Mkongo wa Taifa na Mkurugenzi Mkuu TTCL katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara, yanayofanyika kwenye Viwanja vya Maonesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam. Julai 05, 2023. Kushoto ni Mwana Jiolojia, Erasto Kafyulilo. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Mkurugenzi wa Kampuni ya Imalilo Nutrition Educators katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara, yanayofanyika kwenye Viwanja vya Maonesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam. Julai 05, 2023. Kulia ni Mke wa aliyekua Rais wa awamu ya tatu, Mama Anna Mkapa. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia asali inayozalishwa na Kampuni ya Pinda Honey, katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara, yanayofanyika kwenye Viwanja vya Maonesho ya Sabasaba, Kurasini jijini Dar es Salaam. Julai 05, 2023. Kushoto ni Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza, katika Maonesho ya 47 ya Kimataifa ya Biashara, yanayofanyika kwenye Viwanja vya Maonesho ya Sabasaba jijini Dar es Salaam. Julai 05, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa rai kwa wafanyabishara nchini kutumia maonesho ya kibiashara ya kimataifa ya sabasaba sambamba na fursa za makampuni ya kigeni ili kujifunza na kujipanga kuhudumia masoko makubwa ya ndani, kikanda na kimataifa.
Amesema Ā kufunguka kwa Soko la Eneo Huru la Afrika ā AfCFTA ambalo linakadiriwa kuwa na walaji zaidi ya bilioni 1.3 kutoka nchi 53 barani Afrika ni fursa kubwa kwa wafanyabiashara wa Tanzania.
“Niwaombe wale wote wenye bidhaa zenye viwango na wanaoweza kukidhi vigezo kujisajili kupitia Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ili kunufaika na mpango huo. Ni muhimu sana tukaweka jitihada za dhati kuyafikia masoko haya na siyo kuwa waangaliaji tu na kulalamika.”
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Julai 05, 2023) alipomwakilisha Mheshimiwa Dkt. Rais Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa maonesho ya biashara ya kimataifa ya 47, Temeke Dar es Salaam.
Aidha, amezitaka Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ishirikiane na Wizara ya Kilimo katika kuandaa mpango wa pamoja kuhakikisha uzalishaji unafanyika kwa kuzingatia mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
“Wizara hizi mbili lazima zisomane kiutendaji. Aidha, wataalam wa TanTrade washirikishwe kikamilifu katika kutekeleza majukumu ya utafutaji na ufunguaji wa fursa za masoko ndani na nje ya nchi.”
Mheshimiwa Majaliwa ameipongeza. TanTrade kwa kutenga eneo maalum kwa ajili ya Wamachinga ili na wao wajifunze mbinu za kukua kibiashara.
“Niwasihi wamachinga jifunzeni vizuri teknolojia na mbinu za ufanyaji biashara muweze kukua zaidi.
Amesema ni azma ya Serikali ya Awamu ya Sita kutengeneza mabilionea kupitia Biashara. Pia, ni fahari kubwa kwa nchi kuona wamachinga wanakua na kufanya biashara kimataifa.
Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amezitaka Halmashauri zote nchini kuweka utaratibu wa kuwapanga wamachinga katika maeneo rafiki ya kibiashara, ili wafanye biashara zao kwa uhuru na kuchangia uchumi.
Amesema ni vyema sasa maeneo ya wamachinga yawekewe miundombinu yote muhimu ili kuliinua kundi hilo kutoka wafanyabiashara wadogo kuelekea wakati na hatimaye wakubwa.
Akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni Rasmi, Waziri wa Viwanda na Biashara wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar amesema Wizara zote zitaendelea kushirikiana na kuratibu fursa za wafanyabiashara nchini ili kukuza uchumi.
Awali Naibu Waziri Uwekezaji na Viwanda, Exaud Kigahe amesema Maonesho hayo ni nyenzo muhimu katika kuwakutanisha wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi na kuwapa nafasi ya kutengeneza mitandao ya kubiashara pamoja na kupata masoko ya bidhaa na huduma wanazozizalisha.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Tantrade, Olingeta Mbamba amesema Mamlaka hiyo pamoja na mambo mengine imefanikiwa kushirikiana na Ofisi za Balozi katika nchi za Kenya na Malawi kuratibu wafanyabiashara 206 kutoka Tanzania katika misafara ya kibiashara katika nchi za Sudani Kusini na Malawi ambayo imeweza kutangaza fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade ) Bi Latifa Mohamed amesema Tantrade ndio yenye jukumu la kukuza na kuendeleza Ā biashara Nchini.
“Tantrade inafanya shughuli mbalimbali ikiwemo kufanya utafiti wa masoko wa bidhaa zinazowasilishwa nchini, kutoa taarifa za biashara, kuzijengea uwezo Jumuia za wafanyabiashara juu ya namna bora ya kusimamia shughuli za biashara ndani na nje ya nchi”.
Mwisho