Home LOCAL WAZIRI MKUU AMWAKILISHA RAIS SAMIA URUSI

WAZIRI MKUU AMWAKILISHA RAIS SAMIA URUSI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameondoka nchini leo (Jumatatu, Julai 24, 2023) kwenda Urusi ambako atamwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye Mkutano wa Pili wa Kilele baina ya Wakuu wa Nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi.

Mkutano huo unaotarajiwa kuanza Julai 27 – 30, 2023, utafanyika jijini St. Petersburg, Urusi, na umelenga kuimarisha na kuhamasisha ushirikiano baina ya mataifa ya Afrika na nchi hiyo.

Rais wa Shirikisho la Urusi, Vladimir Putin na Rais wa Comoro, Azali Assoumani, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) wanatarajiwa kuendesha mkutano huo kwa pamoja (Co-Chairing).

Akiwa huko, Waziri Mkuu atashiriki mkutano huo ambao unatarajiwa kukutanisha Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi za Umoja wa Afrika, Urusi, Mawaziri, Mashirika ya Kikanda, Taasisi na Mashirika ya kiserikali kwa kushirikiana na Shirikisho la Urusi.

Aidha Waziri Mkuu atashiriki pia kwenye Jukwaa la Kimataifa la Uchumi na Kibinadamu ambalo limegawanyika katika maudhui makuu manne ambayo ni Uchumi Mpya wa Dunia (the New Global Economy); Usalama Jumuishi (Integrated Security); Sayansi na Teknolojia (Science and Technology); na Masuala ya Kibinadamu na Kijamii (Humanitarian Issues).

Jukwaa hili linatarajiwa kutoa fursa kwa Tanzania kushirikiana na Urusi na mataifa mengine ya Afrika katika kutafuta ushirikiano wa kibiashara, kukuza uchumi na kushughulikia changamoto za maendeleo.

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, JULAI 24, 2023.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here