Home BUSINESS TPDC IMEJIPANGA KUKAMILISHA MIRADI YA GESI ASILIA

TPDC IMEJIPANGA KUKAMILISHA MIRADI YA GESI ASILIA

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Petroli nchini (TPDC) Bw. Mussa Makame Mkurugenzi katika mkutano wa Shirika hilo, wahariri na waandishi wa habari uliondaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina Jijini Dar es Salaam.

Kenneth Mutahongwa Mkurugenzi Utafutaji na Uendelezaji wa Gesi Asilia TPDC akifafanua jambo alipokuwa akitoa mada katika Mkutano huo uliofanyika leo Julai 20,2023 Jijini Dar es Salaam.

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano TPDC, Maria Mselem akizungumza katika mkutano huo.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF) Deudatus Balile(kushoto), akizungumza kwa niaba ya Wahariri waliohudhuria katika Mkutano huo, akitoa neno la shukrani kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina kuwajengea uelewa Wahariri wa Vyombo vya Habari katika sekta ya Mafuta na Gesi.

(PICHA NA: HUGHES DUGILO)

Na: Beatrice Sanga-MAELEZO

Serikali imesema itahakikisha kuwa inakamilisha ujenzi wa miradi ya kuchakata gesi asilia na kuwa kimiminika ili kurahisisha upatikanaji wa nishati hiyo kwa matumizi mbalimbali kwa watanzania, ikiwemo matumizi ya viwandani, kupikia majumbani na nishati ya kuendeshea magari, uzalishaji wa umeme na kukuza uchumi kupitia matumizi ya gesi.

Hayo yameelezwa July 20, 2023 Jijini Dar es Salaam na Mussa Makame Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo la Petroli nchini (TPDC) katika mkutano wa Shirika hilo, wahariri na waandishi wa habari uliondaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ikiwa ni mwendelezo wa taasisi na Mashirika yaliyo chini ya ofisi hiyo kueleza shughuli mbalimbali wanazozifanya.

Makame amesema kuwa katika mradi wa kusindika gesi asilia (LNG) unaotarajiwa kuwekezwa kwa takribani dola za marekani bilioni 42 unalenga kuzalisha, kuchakata na kusindika gesi asilia iliyogunduliwa katika vitalu namba 1, 2 na 4 vilivyopo katika bahari ya kina kirefu katika mkoa wa Lindi na Mtwara unatarajiwa kupunguza changamoto ya nishati nchini.

“Biashara ya gesi asilia haiwezi kukamilika kama gesi hiyo haijachakatwa na kusafirishwa kuwafikia wateja, TPDC kwa kuwezeshwa na serikali imeweza kujenga miundombinu ya kuchakata na kusafirisha gesi asilia kutoka Madimba (Mtwara) na Songo Songo (Lindi) hadi Dar es Salaam, TPDC imeendelea kuhakikisha kuwa watanzania wanaendelea kupata nishati safi ya kupikia pamoja na kuendeshea magari kupitia mfumo wa CNG.” Ameeleza Makame.

Aidha Makame amesema kuwa kwa sasa Shirika hilo linaendelea na ujenzi wa vituo mbalimbali vya kuchakata gesi asilia ili kuhakikisha upatikanaji wa gesi hiyo kwaajili ya matumizi ya vyombo vya usafiri, ikiwemo magari na malengo ni kusambaza vituo vingi nchi nzima ili kurahisisha utapatikanaji wa nishati hiyo kwa karibu zaidi.

“Kwenye suala la matumizi ya gesi kwenye magari na majumbani hapa Dar es Salaam ambacho sasa hivi mradi tunaoutekeleza ni mradi wa kujenga kituo mama (mother CNG station) cha usambazaji wa gesi iliyoshindiliwa (CNG), tunajenga katika eneo la Mlimani City kile kituo kitakuwa kinafanya kazi mbili ambazo ni kushindilia gesi ili itiwe kwenye malori ambayo yatakuwa yanapeleka kwenye vituo dada (daughter CNG tation) ambavyo vitakuwa nje ya pale lakini pia kitakuwa kinajaza magari,” amesema Makame na kuongeza,

“Kingine tunachokifanya ni kutengeneza mpango mkakati wa kuisambaza hii gesi kwenye mji mzima wa Dar es salaam na pia kutoa nje ya Dar es Salaam, huu mpango tunategemea katika miezi 4 mpaka sita ijayo tutakuwa tayari na tutatoa maelekezo yake na utawezesha wawekezaji ambao wamechukua idhini kwetu kwenda kuwekeza kuweza kujua ni eneo lipi zuri ili waweze kuwekeza.” Amesema Makame.

Hata hivyo amefafanua kuwa TPDC imeendelea kutekeleza dira ya kuwa Kampuni ya Taifa ya Mafuta yenye hadhi ya Kimataifa kwa kuendelea na mchakato wa mabadiliko yanayojielekeza katika kupunguza uchafuzi wa hewa (Low carbon emission) sambamba na kuhakikisha kuwa Shirika hilo linajiendesha kibiashara.

Kwa upande wake Deudatus Balile Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF) amesema kuwa Tanzania haina budi kuharakisha upatikanaji wa nishati ya gesi hususani katika matumizi ya magari ili kupunguza uchafuzi wa mazingira na kuongeza mapato kutokana na kuwepo kwa watumiaji wanaohitaji huduma hiyo.

“Asilimia 50 ya uchumi wa Tanzania sasa hivi unakwenda kupatikana kupitia TPDC, Tanzania sasa hivi inatumia sio chini ya Trillion 8 kuagiza mafuta ya dizel, petrol na mafuta ya taa, tukitumia gesi tunaweza tukajikuta kwamba tunapunguza gharama za uagizaji wa mafuta angalau kwa trillion 7 tunabaki kuagiza mafuta ya mitambo mizito na ya uendeshani wa viwanda, kuna uwezekano wa nchi yetu sasa kuwa na kiwanda kikubwa cha kubadilisha magari ambayo yanatumia dizel na petrol kwenda kutumia gesi, tutaweza kutengeneza ajira lakini pia tutatengeneza soko la gesi yetu kwenda katika nchi zitakazokuwa zinabadilisha magari” Amesema Balile.

Balile amewaomba TPDC kujipanga kukopa zaidi fedha ili kuwekeza kwenye miradi mikubwa ambayo itasaidia utegemezi wa nishati kutoka nje ya nchi huku akisema mradi wa LNG ambao utatumia Dola Bilion 42 pamoja na ujenzi wa Bomba la mafuta kutoka Hoima Uganda kwenda Chongoleani Tanga utasaidia kupatikana kwa nishati ya kutosha nchini.

Aidha amesema kuwa TPDC washirikiane na Sekta binafsi katika kuharakisha utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia, na kuendelea kuongeza mtandao wa usambazaji wa gesi asilia kwa njia ya mabomba na gesi iliyoshindiliwa (CNG) kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya gesi asilia katika magari na kupunguza uagizaji wa mafuta ya magari kutoka nje ya nchi

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania ni mkono wa Serikali katika usimamizi wa masuala yote yanayohusiana na utafutaji, uendelezaji, uzalishaji, uchakataji na usambazaji wa nishati za mafuta na gesi asilia

TPDC imeeleza kuwa kupitiwa Ofisi ya Msajili wa Hazina, itaendelea kufanya kazi kwa kasi na kiwango cha hali ya juu na kwa weledi mkubwa ili kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa na Shirika hilo inafanikisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa.
Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here