Home BUSINESS TANESCO MBIONI KUANZA KUTUMIA MITA JANJA

TANESCO MBIONI KUANZA KUTUMIA MITA JANJA

Na: Beatrice Sanga-MAELEZO

SERIKALI imesema kuwa inaendelea na majaribio ya matumizi ya Mita Janja katika kununua umeme nchini huku ikitarajia ndani ya miezi sita ijayo majaribio hayo yatatoa majibu kamili juu ya namna ya kuzitumia na gharama zake.

Hayo yamesemwa July 27, 2023 na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Maharage Chande katika mkutano wa shirika hilo, Wahariri na waandishi wa habari ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina ikiwa ni mwendelezo wa taasisi na mashirika ya Umma yaliyo chini ya ofisi hiyo kueleza shughuli mbalimbali wanazozifanya.

Chande amesema kuwa shirika hilo limedhamiria kuhakikisha linahama kutoka katika mfumo wa manunuzi ya umeme kwa njia inayotumika hivi sasa ambayo inamwezesha mtumiaji wa umeme kununua umeme akiwa eneo la nyumbani pekee ndipo anaweza kuweka umeme na kuhakikisha watu wanatumia Mita Janja katika manunuzi ya umeme ambazo zinamwezesha mtumiaji wa umeme akiwa mahali popote kwa kutumia mfumo huo.

“Mita janja zitawezesha kuingiza umeme siyo lazima ukiwa nyumbani kwako, kwa hiyo tukaanza tathmini ya kuhama mfumo, kutoka mfumo wa sasa kwenda Mita janja na matokeo ya tathmini ya hiyo yametoka na tayari kwa sasa kuna Mita Janja ambazo tunazijaribu kwa maana ya approval of consent na zinafanya kazi, changamoto tuliyoipata ni kwamba gharama za mita janja ni kubwa sana, mita janja ili zifanye kazi lazima ziongee na sisi kwa maana ya kutoka kwenye mita kuja kwetu ili uweze kuingiza remote ambayo inakuja na gharama zake.” Amesema Chande.

Chande amesema kwa sasa Tanesco inaendelea na mazungumzo na wakandarasi mbalimbali kuona namna bora ya kuimarisha mfumo huo na kumpunguzia gharama mtumiaji wa mwisho wa mfumo huo ambaye ni mteja.

“Watu wetu wamegundua njia mbadala kwa hiyo tutawahusisha wakandarasi wa mita za sasa hivi kuangalia kama tunaweza kwenda kwenye Mita Janja, siyo kwa kutumia gharama kubwa ila kwa kutumia nyaya zetu za umeme ili yule mteja wa mwisho asiwe na gharama za kulipa, ukiongeza gharama hata mafanikio ya hiyo mita janja hayatokuwepo kwahiyo ni matumaini yetu ndani ya miezi sita tutaweza kuwa tumekamilisha hizo mbinu mpya na kuanza kusambaza mita janja.” Amefafanua Chande.

Aidha, amesema kuwa kwa sasa ili mtumiaji aweze kuutumia mfumo wa mita janja ni lazima awe na kadi ya simu ambayo ni lazima iwe na kifurushi kuweza kuitumia hivyo anaamini kuwa utakuwa mzigo mzito kwa mtumiaji hivyo wameamua kutumia optical fiber ili mteja wa mwisho asiwe na gharama kubwa za kulipa.

“Kwa sababu ile mita ili iweze kuongea ni lazima utumie simcard na ili utumie simcard lazima utumie bando na bando lazima ulipie kwa hiyo nani analipa hilo bando analipa mteja ama analipa TANESCO? hiyo bado changamoto, hivyo tatizo siyo teknolojia, tatizo ni gharama na nani atazichukua hizo gharama,” ameeleza Mkurugenzi huyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF), Deodatus Balile amesema kuwa mabadiliko yanayofanywa na Shirika la umeme Tanzania nchini ikiwemo kuongezeka kwa mauzo ghafi ya umeme, usimamizi mzuri wa uendeshaji wa shirika hilo pamoja na kushughulikia changamoto ya mgao wa umeme ambao umekuwa ukitoka mara kwa mara hayana budi kuungwa mkono.

“Kuna moyo mpya wa kujituma, kuna fikra mpya za kujituma zinazoingizwa serikalini kutoka sekta binafsi, kasi ya mabadiliko inayofanywa ndani ya Tanesco inadhihirisha kuwa kumbe tukijenga fikra mpya mambo haya yanawezekana, Tanesco kutoka shirika la kupata hasara, shirika ambalo ulikuwa ukipiga simu unatukwanwa, lakini leo Tanesco ukipiga simu kwamba nguzo imeanguka mita imeleta shida umeme haupo ndani, wana Bajai, wana pikipiki na magari, watakufikia na kutanzua hilo tatizo, hii inadhihirisha kuwa siyo kwamba mambo haya yanawezekana Ulaya hata kwa nchi zetu hizi yanawezekana kinachohitajika ni usimamizi mkubwa,”

Tanesco imeeleza kuwa kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, itaendelea kufanya kazi kwa kasi na kiwango cha hali ya juu na kwa weledi mkubwa ili kuhakikisha miradi yote inayotekelezwa na Shirika hilo inafanikisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here