Home LOCAL SERIKALI KUENDELEA KUWATAMBUA WABUNIFU ILI KUKUZA MAENDELEO MAENDELEO UCHUMI

SERIKALI KUENDELEA KUWATAMBUA WABUNIFU ILI KUKUZA MAENDELEO MAENDELEO UCHUMI

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga (katikati), akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa udahili  na Menejimenti ya Data Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), Dkt. Kokuberwa Katunzi (kushoto) alipotembelea banda la TCU wakati wa kufunga Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyomalizika leo Julai 22, 2023 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa.
WIZARA ya Elimu Sayansi na Teknolojia imesema inaendelea kuwatambua wabunifu nchini kwa lengo la kuchagiza maendeleo ya uchumi na kijamii ikiwa ni pamoja na kubidhaisha teknolojia na ubunifu na kuongeza ufanisi katika kuchangia uchumi.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga ameyasema hayo Leo Julai 22,2023 wakati akifunga maonesho ya 18 ya vyuo vikuu yaliyoandaliwa na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).
Maonesho hayo yana  kaulimbiu ya “Kukuza ujuzi nchini kupitia elimu ya juu, Sayansi na Teknolojia kwa uchumi imara na shindani .
Amesema Wizara imetoa mafunzo kwa wabunifu wachanga 83 na kutoa rasilimali fedha kwa wabunifu 23 ili kuendeleza bunifu na teknolojia zao ili zifikie hatua ya biashara.
Pia amesema kuwa hivi sasa wanaishi katika ushindani mkubwa si tu wa kiuchumi na kijamii bali pia ubunifu wa teknolojia mpya na uvumbuzi wenye lengo la kuboresha na kurahisisha maisha.
Amesema kuwa taasisi za elimu zina mchango mkubwa katika kuleta mageuzi ya elimu kwa kuhakikisha wahitimu wanapata ujuzi na maarifa stahiki na shindani katika soko la ajira na kuhimili ushindani wa Kikanda na Kimataifa.
Ameeleza kuwa taasisi hizo zinapaswa kujielekeza katika matumizi ya teknolojia na ubunifu kama ilivyoainishwa katika mpango wa tatu wa taifa wa maendeleo wa miaka mitano wa 2021/22 na 25/26.
“Mpango huu unasisitiza na kuhimiza matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu hususan matumizi ya takwimu, mitambo inayoendesha kompyuta na roboti. Ninaamini taasisi za elimu ya juu watatekeleza na kutimiza  adhma ya serikali,” amesema Kipanga.
Ameongeza kuwa mpango huo ni nyenzo muhimu ya kuchochea na kukuza maendeleo ya sayansi na teknolojia hivyo, alizitaka taasisi hizo kuelekeza tafiti na bunifu katika maendeleo.
Kwa mujibu wa Kipanga, wataendelea kuwaendeleza na kuwatambua wabunifu sambamba na kubidhaisha ubunifu kwa lengo la kutatua changamoto za kijamii.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa tume hiyo, Makenya Maboko amesema wamekuwa wakiandaa maonesho hayo tangu mwaka 2016 na kwamba malengo ya maonesho hayo ni kutoa fursa kwa vyuo vya elimu ya juu kutangaza huduma na kazi wanazofanya katika ustawi wa elimu hiyo nchini.
Amesema kuwa wanalenga kujenga na kuimarisha mahusiano baina ya taasisi za elimu ya juu na kutoa fursa kwa wananchi na wadau kuona shughuli zao ikiwemo programu za masomo hivyo kufanya maamuzi na chaguzi sahihi wanapohitaji kujiendeleza kitaaluma.
“TCU itaendelea kutekeleza majukumu yote ya serikali kama yalivyoainishwa katika sera, mipango na mikakati mbalimbali ya maendeleo ya nchi yetu katika masuala yote yanayohusu maendeleo ya elimu ya juu,” Amesema Maboko.
Pia amesema watahakikisha wanaimarisha mifumo ya udhibiti ubora ya ndani ya vyuo vikuu ili waweze kutoa elimu inayokidhi mahitaji, viwango vya ubora kimataifa, Kikanda na kuzifanya taasisi zao kuwa chachu ya maendeleo ya taifa.
Amesisitiza kuwa maonesho hayo yataendelea kuwa chachu ya kuongeza fursa za masomo ya elimu ya juu kwa wahitimu wa ndani na nje ya nchi, kuchagiza ushindani baina ya taasisi na kuinua viwango vya ubora.
Maboko amesema wataongeza tija ya maonesho hayo kwa jamii, taasisi zinazoshiriki na wageni wanaotembelea maonesho.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga akizungumza  na wadau mbali mbali wa Elimu wakati wa kufunga Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyomalizika leo Julai 22, 2023 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga (katikati), akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi inayosaidia wanafaunzi kusoma nje ya nchi (Universities Abroad Representative) alipotembelea banda la UAR wakati wa kufunga Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyomalizika leo Julai 22, 2023 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Omary Kipanga akizungumza na watumishi kutoka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) wakati wa kufunga Maonesho ya 18 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yaliyomalizika leo Julai 22, 2023 katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here