* Wamo pia Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu kutoka nchi mbalimbali
* Ashangiliwa kwa kuhutubia wageni wa nje kwa Kiswahili
Na: Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Samia Suluhu Hassan ameendelea kuipaisha Tanzania kimataifa baada ya kufanikisha ujio jijini Dar es Salaam wa marais wasiopungua sita na Makamu wa Rais na Mawaziri Wakuu kadhaa kutoka nchi mbalimbali duniani.
Viongozi hao waliwasili Tanzania kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu Rasilimali Watu (Africa Heads of State Human Capital Summit) uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam, leo tarehe 26 Julai, 2023.
Marais waliowasili Dar es Salaam ni pamoja na Rais William Ruto wa Kenya, Rais Andry Rajoelina wa Madagascar na Rais Carlos Vila Nova wa São Tomé na Principe.
Rais wa Sierra Leone, Julius Maada Wonie Bio, Rais Filipe Nyusi wa Msumbiji na Rais wa Malawi, Dkt. Lazarus Chakwera, pia ni miongoni mwa marais waliokuja Tanzania.
Makamu wa Rais, Mawaziri Wakuu na wageni wengine mashuhuri kutoka Uganda, Rwanda, Sudani Kusini, Namibia na nchi nyingine nao wamekuja Dar es Salaam kuhudhuria mkutano huo.
Akiwa ni mwenyeji wa marais hao, Rais Samia pia alifanya mazungumzo ya pembeni na baadhi ya viongozi ili kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na mataifa ya nje.
Rais Samia aliwakosha wajumbe wa mkutano huo kutoka nchi mbalimbali za Afrika na kwingine duniani baada ya kuamua kuhutubia kwa kutumia lugha ya Kiswahili, kitendo kilichofanya ashangiliwe na wahudhuriaji wa mkutano huo.