Home LOCAL RAIS SAMIA ARIDHIA HEKTA 18,031 KUTOLEWA KWA WANANCHI RUTORO

RAIS SAMIA ARIDHIA HEKTA 18,031 KUTOLEWA KWA WANANCHI RUTORO

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (wa pili kushoto), Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (wa tatu kushoto) na mkuu wa mkoa wa Kagera Fatma Mwassa (Kushoto) wakimsikiliza mmoja wa wawekezaji wa Ranchi  ya Kagoma mkoani Kagera wakati wa ziara ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta wilayani Muleba tarehe 20 Julai 2023.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati wa ziara ya Mawaziri wa Wizara za kisekta Rotoro wilayani Muleba mkoa wa Kagera tarehe 20 Julai 2023.

Sehemu ya wananchi wa Rutoro wilayani Muleba mkoa wa Kagera wakifuatilia hotuba za Mawaziri wa Wizara za Kisekta walipokwenda kutoa mrejesho wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na mgogoro wa Matumizi ya ardhi katika eneo hilo tarehe 20 Julai 2023.

Sehemu ya wananchi wa Rutoro wilayani Muleba mkoa wa Kagera wakifuatilia hotuba za Mawaziri wa Wizara za Kisekta walipokwenda kutoa mrejesho wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na mgogoro wa Matumizi ya ardhi katika eneo hilo tarehe 20 Julai 2023.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Khamis Hamza Chillo akizungumza wakati wa mkutano wa Mawaziri wa Wizara za Kisekta katika eneo la Rutoro Muleba mkoa wa Kagera tarehe 20 Julia 2023.

Abdallah Ulega, Waziri wa Mifugo na Uvuvi akisisitiza jambo katika mkutano wa Mawaziri wa Wizara za Kisekta eneo la Rutoro Muleba mkoa wa Kagera tarehe 20 Julia 2023.

Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde akizungumza kwenye   mkutano wa Mawaziri wa Wizara za Kisekta katika eneo la Rutoro Muleba mkoa wa Kagera tarehe 20 Julia 2023.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Lucy Kabyemera (wa pili kushoto) akiwa katika mkutano wa Mawaziri wa Wizara za Kisekta eneo la Rutoro Muleba mkoa wa Kagera tarehe 20 Julia 2023. (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)

Na: Munir Shemweta, WANMM MULEBA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan ameridhia kumegwa eneo la Ranchi ya Kagoma iliyopo wilaya ya Muleba DC na Karagwe mkoani Kagera yenye ukubwa wa hekta 18,031.26 kwenda kwa wananchi kuendelea na shughuli mbalimbali za kibinadamu ikiwemo makazi.

Hayo yamebainishwa tarehe 20 Julai 2923 katika kijiji cha Rutoro wilayani Muleba mkoa wa Kagera na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa kutoa mrejesho wa Maamuzi ya Baraza la Mawaziri kuhusiana na utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 kwa wananchi wa Rutoro.

Kufuatia kumegwa eneo hilo, wananchi wa Rutoro watakuwa wamepata asilimia 44.44 kutoka asilimia 100 ya Ranchi ya Kagoma huku asilimia 55.56 ikibaki katika ranchi hiyo ambapo Waziri wa Ardhi Dkt Mabula alisema kinachokwenda kuwatenganisha wawekezaji na wananchi baada ya maamuzi hayo ya serikali ni mipaka mipya itakayowekwa

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, vijiji ambavyo wananchi wake watanufaika na uamuzi huo  ni Rutoro, Kyobuheke, Mishambya pamoja na Byengeregere.

‘’Serikali haijafanya makosa kufanya maamuzi hayo bali ni utaratibu unaolenga kuwapunguzia adha waliyokuwa nayo wawekezaji kwa kugombana na wananchi na mheshimiwa Rais hapendi hayo madhara yanayotokea kwa pande zote ndiyo maana uamuzi umechukuliwa kuwatenganisha’’ alisema Dkt Mabula.

Alisema, utaratibu uliotumika kutoa maeneo kwa wananchi katika kata ya Rutoro utasaidia kumaliza tatizo la Mwisa II kwa kuzingatia mapendekezo ya mkoa wa Kagera.

Mbunge wa Jimbo la Muleba Kaskazini Charles Mwijage mbali na kupongeza uamuzi huo wa serikali alionya wananchi wa Rutoro kuepuka kukaribisha watu mara baada ya uamuzi huo na kuwataka kutulia kuisubiri serikali iwapatie vitu walivyovikosa.

Kwa upande wake Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega amewataka wananchi kutovamia maeneo ya watu wengine hasa baada ya uamuzi huo na kueleza kuwa, kufanya hivyo ni kuingia katika hatia na serikali itachukua hatua kwa watakaofanya hivyo.

‘’Msivamie eneo la mtu yeyote hadi utaratibu utakapokuwa umekamilika na yaliyotangazwa hapa hayamfanyi mmoja kati yetu atoke aende kujimilikisha, atakayefanya vitendo visivyokuwa vya kiuungwana kwa kuvamia eneo hatakuwa na mtetezi kutoka upande wowote’’ alisema Ulega.

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Khamis Hamza Chilo amewataka wananchi wa Rutoro kuhakikisha wanapanda miti kwenye maeneo wanayoenda kuishi ili kutunza mazingira sambamba na kuondokana na athari ya tabia nchi.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kagera Nazir Karamagi alisema,  amefurahishwa na ziara ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta katika mkoa wake na kueleza kuwa ujumbe huo umekwenda na mamlaka kamili na kufanya maamuzi waliyokubaliana kuhusiana na utatuzi wa mgogoro wa matumizi ya ardhi katika eneo hilo.

Naye Anthony Mavunde, Naibu Waziri wa Kilimo alieleza kuwa, anaamini baada ya mpango wa matumizi bora ya ardhi kuwekwa kwenye eneo waliopatiwa wananchi na hatimaye wakulima kupangwa vizuri basi utaratibu wa miradi ya umwagiliaji utapelekwa na wakulima watanufaika  na miradi hiyo.

Kamati ya Mawaziri wa Wizara za Kisekta iliyohusisha Mwaziri kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mifugo na Uvuvi, Kilimo, Maliasili na Utalii, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) pamoja na Makatibu Wakuu wa Wizara hizo na wale wa Maji, TAMISEMI na Ulinzi imehitimisha ziara yake ya siku moja katika mkoa wa Kagera ikiwa ni muendelezo wa juhudi za kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here