Home LOCAL PROGRAMU YA MABADILIKO YA KIUTENDAJI KWA WATAALAM KUSAIDIA UBORESHAJI WA UBORA WA...

PROGRAMU YA MABADILIKO YA KIUTENDAJI KWA WATAALAM KUSAIDIA UBORESHAJI WA UBORA WA HUDUMA ZA AFYA

Na: Englibert Kayombo, Dodoma.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa katika Vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa kuanzisha Programu ya mabadiliko ya kiutendaji kwa wasimamizi na watoa huduma za afya (Leadership4 Health Transfomation Program) katika vituo vya umma vya kutolea huduma za afya.

Waziri Ummy amesema Serikali imeboresha Huduma za afya kuanzia ujenzi wa miundombinu ununuzi wa dawa, vifaa, vifaa tiba, vifaa vya maabara, kuajiri na kusoimesha wataalamu kwa lengo la kuboresha Huduma za afya nchini.

Hivyo uongozi na usimamizi mzuri ndani ya sekta ya afya ndio suluhisho la kufikia lengo la ubora wa Huduma za afya kwa wananchi.

Waziri Ummy amesema hayo kupitia ukurasa wake wa twitter Julai 20, 2023 akiwa anawapongeza Taasisi ya Mifupa Mo Taasisi ya Mifupa (MOI) kwa kuanzisha utaratibu wa kuwapigia simu wagonjwa wao ili kupata maoni, ushauri, pamoja na kuwajulia hali kuwa ni jambo la mfano na linafaa kuigwa na taasisi zote za kutolea huduma za afya.

“Hongereni Taasisi ya Mifupa (MOI) pasi na shaka MOI chini ya Uongozi wa Prof. Abel Makubi inakwenda kuwa nzuri zaidi, serikali kwa upande wetu imefanya mengi kuboresha Huduma za afya na sasa tunajikita katika kuboresha ubora wa Huduma za afya nchini”, ameeleza Waziri Ummy

Mnamo Tarehe 12, Mwezi Mei, mwaka huu, Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akiwa anawasilisha hoja kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania la kuridhia na kupitisha Bajeti ya Wizara ya Afya kwa mwaka wa fedha 2023/24 mnamo tarehe 12 Mwezi Mei 2023, Mhe.Ummy aliliomba Bunge kupitisha bajeti ya shilingi 1,235,316,516,000 ili Wizara ya Afya iweze kutekeleza kikamilifu vipaumbele 14 vya kuimarisha ubora wa huduma za afya nchini.

Miongoni mwa Vipaumbele hivyo ilikuwa ni ‘Kuboresha ubora wa huduma zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini kwa kuanzisha programu ya mabadiliko ya kiutendaji kwa wasimamizi na watoa huduma za afya’ (Leadership4Health Transfomation Program)

Alieleza kuwa Serikali imeboresha miundombinu, kuajiri wataalamu na kununua vifaa tiba na dawa sasa ni wajibu wa watoa huduma za afya nchini kufanya kazi kwa uzalendo, weledi na ufanisi wa hali ya juu ili kuweza kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.

“Programu hii italenga kuleta mabadiliko ya utendaji kazi wa watumishi wa afya katika vituo vya kutolea huduma afya kwa kuwapima ufanisi wao katika utendaji kazi”, alifafanua Waziri Ummy.

“Tutaanzisha utaratibu wa kupima utendaji wa timu za uendeshaji wa huduma za afya katika ngazi za Vituo, Hospitali, Halmashauri (CHMT) na Mikoa (RHMT) katika maeneo ya maoteo ya dawa, upatikanaji wa dawa, huduma za uchunguzi (maabara na Radiolojia) udhibiti wa kuchina na kuchotora wa dawa, taratibu za kushughulikia malalamiko ya wagonjwa, muda wa kuwahudumia wagonjwa” alisisitiza Waziri Ummy.

Alisema kuwa Serikali itaendelea kuimarisha utawala bora, uongozi na menejimenti ya usimamizi wa huduma za afya kwa kushirikisha Kamati za Ulinzi na Usalama na Viongozi na Watendaji wa Serikali katika ngazi zote pamoja na kufanya kaguzi za mara kwa mara pamoja na kuimarisha usimamizi shirikishi katika vituo vya kutolea huduma za afya.

“Tuhakikisha utoaji wa huduma za afya unazingatia weledi, maadili na miiko kupitia mabaraza ya kitaaluma na bodi za usajili ikiwemo kuanzisha mfumo wa kuwatambua na kuwapa tuzo wataalam wanaofanya vizuri” alisema Waziri Ummy.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here