Home LOCAL NI JUKUMU LA WAAFRIKA WENYEWE KUTUMIA IDADI KUBWA YA VIJANA KWA MAENDELEO...

NI JUKUMU LA WAAFRIKA WENYEWE KUTUMIA IDADI KUBWA YA VIJANA KWA MAENDELEO YA NCHI ZAO

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi SMZ Dkt. Hussein Mwinyi akitoa hotuba ya shukurani katika mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika uliokuwa unajadili kuhusu mtaji wa rasilimali watu jijini Dar es Salaam. 

Baadhi ya wakuu wa nchi za Afrika wakiwa katika majadiliano ya mkutano huo kwenye ukumbi wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan akitoa mchango wake katika mjadala huo kwenye mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika uliojadili kuhusu Rasilimali watu. 

Na Sophia Kingimali

Mkutano wa siku mbili wa wakuu wa nchi za Afrika wenye lengo la kujadili kuhusu mtaji wa rasilimali watu umehitimishwa Leo Julai 26 na kupitisha Azimio la Dar es Salaam la rasilimali watu la Bara la Afrika lenye lengo la kuangazia mkakati wa kuboresha Elimu bora, Afya, Uwezeshaji wanawake kiuchumi na kijamii, Ubia kati ya Serikali na wadau wengine, Sera jumuishi, Ajira na Usawa wa kijinsia ambapo Rais Mwinyi amesema ni jukumu la waafrika kupanga mustakabali kwa kuhakikisha kwamba uwepo wa idadi kubwa ya vijana katika nchi hizo unakuwa na faida. Huku wakuu wa Nchi za Afrika wakisaini na kupitisha azimio hilo.

Azimio hilo limesomwa leo Julai 26 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan wakati wa hitimisho la mkutano huo.

Kwa upande wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi wakati akitoa neno la shukrani baada ya kufungwa kwa mkutano huo, amewataka Viongozi wa nchi za Bara la Afrika kutekeleza mikakati iliyojadiliwa katika mkutano wa Wakuu wa Nchi hizo kuhusu Rasilimali Watu, kuwa na mtazamo wa Pamoja katika kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi hizo.

“Naomba nimalizie kwa kutoa wito wa utekelezaji wa azimio la Dar es Salaam, nawaasa washiriki wa mkutano huu kuchukua maarifa na uzoefu uliopatikana ili kuutumia katika kendeleza rasilimali watu kwenye nchi zetu, kwa pamoja tuanze safari ya kutekeleza mikakati iliyojadiliwa na kuwa na mtazamo wa pamoja katika kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi wa Afrika na kuongeza tija ya vijana kupitia elimu bora katika stadi za kazi

Ni juu yetu kama waafrika kupitia kizazi hiki kupanga mustakabali wetu kwa kuhakikisha kwamba uwepo wa idadi kubwa ya vijana katika nchi zetu unakuwa na faida kwetu badala ya kuwa mzigo kwetu” amesema Rais Mwinyi.

Rais Mwinyi amesema mkutano huo umetoa fursa muhimu za kujadili na kutatua changamoto ambazo zinalikabili Bara la Afrika hivyo anaamini Benki ya Dunia ambayo imefadhili mkutano huo kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania itaendelea kutekeleza Azimio la Dar es Salaam lililopitishwa na wakuu  hao wa nchi.

Aidha ameongeza kuwa mijadala iliyofanyika ni kipimo tosha cha kuwekeza katika elimu na afya na  kutafuta soko la ajira kwa vijana.

Katika azimio hilo wakuu wa nchi wataenda kutimiza ahadi na kuendeleza azimio la Dar es Salaam kuhusu umuhimu wa Afya, Elimu, Usawa wa kijinsia na ajira ambapo hadi kufikiwa kwa maazimio hayo kunatokana na uwepo wa changamoto ziunazolikabili bara la Afrika.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here