Home LOCAL ‘MWAKA 2023/2024 MSALALA TUNA MALENGO MAKUBWA’

‘MWAKA 2023/2024 MSALALA TUNA MALENGO MAKUBWA’

Mkurugernzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala mkoani Shinyanga, Khamis Katimba amesema, halmashauri hiyo imepanga kuvuka lengo la makusanyo ya mapato yaliyokusanywa katika Mwaka wa Fedha 2022/23.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii kuhusu matarajio yake kwenye halmashauri hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 amesema, baada ya kuwa na kikao cha pamoja na watendaji wenzake, wameona kuna mazingira mazuri ya kuongeza kiwango cha makusanyo katika mwaka wa mpya fedha.

“Kwenye mwaka wa fedha 2022/23 halmashauri ilikusanya zaidi ya Bil. 5.36 na tulipata hati safi, lakini baada ya kukaa na watendaji wenzangu, tumeona upo uwezekano wa kwenda juu zaidi katika Mwaka wa Fedha 2023/24.

“Madiwani wa halmashauri yetu wamekuwa wakishirikiana kwa kiwango cha karibu mno, ndio maana halmashauri ilipata hati safi na ninaamini ushirikiano huu utaendelea kwa kuwa ndio nguzo ya mafanikio hapa kwetu,” amesema Katimba.

Mkurugenzi huyo amesema, Msalala ina fursa mbalimbali ikiwa ni pamoja na kilimo cha mpunga, dengu sambamba na biashara ndogondogo na kushauri wananchi kuchangamkia fursa hiyo ya kilimo.

“Pia Mgodi wa Barrick Bulyanhulu ni fursa kubwa kwa wananchi wetu, tunao wajibu wa kuwaonesha njia ya kufaidika zaidi lakini namna wanavyoweza kujiongezea kipato kutokana na Barabara Kuu iendayo Mwanza na Geita.

“Tunayo mradi wa viwanja katika maeneo ya Kata za Isaka, Segese, Kakola na Bulige ambapo tunawaomba wananchi wachangamkie, haya ni maeneo ya kimkakati yaliyopimwa na yenye huduma muhimu,” amesema.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mibako Mabubu amepongeza jitihada zinazofanywa na madiwani wa halmashauri hiyo na kushauri kushirikiana karibu na mkurugenzi huyo ili kufikia malengo.

“Tunaamini tutafika mbali kwani baada ya kikao na mkurugenzi wetu, tumeona mikakati yake ambayo inatekelezeka.

Ushirikiano wetu ndio nguzo pekee ya kusaidia halmashauri yetu,” amesema Mabubu.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here