Home LOCAL KINANA: RAIS SAMIA HAWEZI KUUZA BANDARI

KINANA: RAIS SAMIA HAWEZI KUUZA BANDARI

MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdurhaman Kinana, amezungumzia mjadala wa uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam huku akiweka wazi kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan na Serikali anayoingoza haiwezi kuuza bandari hiyo na kuhoji Rais auze bandari kwa maslahi yapi.
 
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Mkendo Musoma Mjini Kinana alianza kwa kueleza kuwa liko jambo la bandari linazungumzwa na mjadala mkubwa, unaendelea kuwa mrefu, mjadala mpana.
 
“Nataka niwahakikishie msiamini kwamba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyekula kiapo eti atafanya jambo ambalo halina maslahi na nchi. Haiwezi kutokea, Rais ambaye tangu amechukua usukani amefanya mambo mengi mazuri, kwa nini aende kuuza bandari, sababu ni ipi?
 
“Ili apate nini, ili iweje na ukisikiliza huu mjadala usikilizeni kwa makini na mmeshausikiliza, wote tunaoutetea, wanaopinga pamoja na wanaokosoa hakuna anayesema kwamba kusiwe na uwekezaji hata mmoja kwani wote wanakubali kwamba kuna haja ya kuwekeza  na lengo ni moja tu kuongeza ufanisi na kuongeza mapato.
 
“Serikali imesema tunakwenda kufanya kazi hii kwa nia njema ya kuongeza ufanisi, kuongeza mapato tuweze kufanya shughuli nyngi zaidi za maendeleo. Wamejitokeza watu wameanza kuhoji, wako wanaohoji kwa nia njema ya kujenga ya uzalendo, hatuwezi kusema kila anayehoji anania mbaya,” alisema.

Aliongeza wako wanaotetea mkataba na wametoa ushauri mzuri, serikali imesema itapokea kila ushauri utakaotolewa, Chama Cha Mapinduzi kimesema serikali isikilize, kwa hiyo serikali inasikiliza ushauri, inasikiliza hoja, haya yote yatafanyiwa kazi, haiwezekani Rais akapuuza haya yote.
 
“Kiongozi mzuri ni yule ambaye panapotokea ubishani, watu wanabishana na hoja mbalimbali znatolewa anatulia, anasikikiza.
 
“Anachofanya Rais ni kuwa mtulivu kusikiliza kila hoja kuchambua kila hoja, kutathimini kila hoja, ili muda utakapofika tupate uwekezaji ulio bora zaidi kwa manufaa ya Watanzania. wako waliopeleka mjadala huu katika udini, wengine katika muungano Bara na Visiwani, hakukua na sababu,”alisema Kinana.
 
Alifafanua kuwa uwekezaji huo ni wa kiuchumi hivyo unatakiwa kujadili kwa hoja,hoja itasikilizwa, hoja yako itajibiwa , pale itakapotakiwa kufanyiwa kazi itafanyiwa kazi kwa maslahi mapana ya nchi.
 
“Sasa niseme yafuatakayo hakuna anayekataa ,wale wanaopinga na wanaonga mkono, hakuna anayekataa uwekezaji , Serikali inaendelea kusiliza hoja ,maoni na hofu zinazotolewa.
 
“Chama chetu kimeagiza kwamba wananchi wasikilizwe kwa kila ngazi , kwa kila sehemu, Serikali inaendelea kusikiliza.Sina mashaka hata kidogo kwamba Rais atatoa uamuzi wa busara katika jambo hili na hata uamuzi huu alipoufikia kuwekeza katika  Bandari ni kwa sababu moja tu ya maslahi mapana ya watanzania na nchi sio kwasababu nyingine yoyote.
 
“Najua tuko watu wengi tuko vyama vingi ndio wakati muafaka sasa likitokea jambo kila mtu anatatafuta namna ya kulitengeneza kwa namna ambayo linakuwa na manufaa kwake. Kwa hiyo ukipiga kelele sana nchi imeuzwa …imeuzwa …imeuzwa ungependa watu waamini kwamba imeuzwa.
 
“Hakuna bandari inauzwa, inauzwaje? kwanini iuzwe ?Bandari ya Musoma hapa inauzwaje”, kwa bei ipi ? kwasababu ipi? Ili iwe vipi hakuna sababu, naomba tuwe watulivu. Naomba tuwe na imani na Serikali yetu tuwe na imani na Rais wetu ,tumuamini kwamba kila jambo analofanya ni kwa maslahi ya Taifa letu .

Awali   wabunge wa Mkoa wa Mara wanaotokana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na kumpongeza Rais Samia kutokana na kupeleka maendeleo katika mkoa huo pia wanaendelea kumuunga mkono katika jitihada mbalimbali anazoendelea kuchukua kuhakikisha nchi yetu inapiga hatua huku wakizungumzia suala la uwekezaji katika Bandari ya Dar es Salaam ambapo wameomba wananchi kutosikiliza maneno ya upotoshaji yanayotolewa na baadhi ya kikundi cha watu.
 
Kwa upande wake Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa(NEC) ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Homud Abuu Jumma alitumia nafasi hiyo kusisitiza kuwa bandari haijauzwa bali bandari imewekezwa na faida kubwa ipo kubwa.
 
“Nichukue fursa hii kuipongeza Serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais samia Suluhu Hassan, Serikali imefanya mambo makubwa tena tunatakiwa kuandika kwa wino wa dhahabu ambao hautafutika. Wakati Rais Samia anaingia madarakani kuna watu walikuwa na mashaka makubwa lakini leo wanajionea mambo yanakwenda.
 
“Kuna miradi ilikuwa imeanza na wakawa wanadhani miradi itakwama lakini leo inakwenda vizuri na mingine imekamilika, miradi ya kimkakati yote inaendelea, kuna bwawa la Mwalim Nyerere ambalo linafaida kubwa na likianza  kuzalisha umeme utapatikana wa kutosha na bei itashuka,”alisema
 
Mbunge Viti Mkoa wa Tabora Munde Tandwe alieza kuna genge la wahuni wanapita mtaani wakisema nchi imeuzwa wakati wanajua Rais Samia hawezi kuuza, Rais ameleta maendeleo katika kila eneo, wanaoneza propaganda na wamekosa hoja ya kueleza kwa wananchi.
 
Aidha alitumia nafasi hiyo kutoa ombi kwa wana CCM wanaotaka Ubunge na Udiwani wacheni wabunge na madiwani walioko madarakani wafanye kazi zao, muda ukifika watapewa nafasi.
 
“Acheni wabunge wafanye kazi zao, unapoingia kwenye jimbo mapema unafanya mbunge au diwani aliyekuwa madarakani ashindwe kutekeleza miradi ya maendeleo na kutumia muda mwingi kutetea jimbo lake.Acheni kuingilia wabunge wanaotekeleza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi.”
 
Wakati huo huo Mjumbe wa Halmashauri Kuu(NEC) ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) Richard Kasesela aliwaomba wananchi kutowasikiliza wapinzani ambao wamekuwa wakifanya mikutano ya hadhara na kupotosha wananchi kuhusu uwekezaji wa bandari ya Dar es Salaam.
 
“Kuna watu walifanya mkutano hapa wakaeneza uongo mkubwa, wakidai eti mradi wa uwekezaji katika bandari ya Dar es Salaam hauna maslahi lakini ukweli mradi unafaida kubwa na hakuna hasara na wakipewa wawekezaji bali faida itakuwa kubwa.Kuna watu waliofungua kesi, lakini wasikae nyuma wajitokeze hadharani badala ya kujificha.Wanasema bandari zote zimechukuliwa hapa Mara bandari yenu imechukuliwa?Si ipo na mnaitumia.”
 
Mwisho

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here