Home BUSINESS KENYA YAIPONGEZA STAMICO, YAAHIDI KUENDELEA KUJIFUNZA KWAKE

KENYA YAIPONGEZA STAMICO, YAAHIDI KUENDELEA KUJIFUNZA KWAKE

        

Na Beatrice Sanga-MAELEZO

Kenya imefurahishwa na utendaji kazi wa Shirika la Madini Nchini (STAMICO) pamoja na Wizara ya Madini kwa ujumla, hivyo imeahidi kuendelea kujifunza ili kuhakikisha inakuwa na uendelezaji mzuri na uchimbaji wa rasilimali madini nchini humo.

Hayo yameelezwa July 22, 2023 na Elijah Mwangi Katibu Mkuu Wizara ya Madini na Uchumi wa Bluu nchini Kenya wakati wa ziara yake na ujumbe wake kutoka nchini humo waliokuja kujifunza na kuona jinsi STAMICO na Wizara ya Madini kwa ujumla wanavyofanya shughuli zake na kutembelea baadhi ya maeneo ya migodi hapa nchini ambapo pia ameeleza wamefurahi kuwepo Tanzania kutokana na ushirikiano waliopewa ambao umewawezesha kujifunza vitu vingi.

Mwangi amesema kuwa wataendelea kujifunza namna ambavyo STAMICO wamefanikiwa kuendesha shughuli za madini katika kugundua, uchimbaji wake, kuendeleza sekta hiyo pamoja na mengine mbalimbali yanayohusu sekta hiyo ambapo anaamini kuwa kwa sasa Tanzania inanufaika vya kutosha kutokana na rasilimali hizo.

“Tumejifunza mambo mengi kwa jinsi gani madini yanaweza kubadilisha maisha ya wanajamii na Taifa kwa ujumla, tumekuja hapa na wajumbe kutoka Shirika la taifa la Madini la Kenya ili waweze kujifunzaa, kwasababu sisi bado ni shirika changa ambalo hatuwezi kujilinganisha na STAMICO ambalo limeanza muda mrefu, na hatukuona sababu ya kuchagua nchi nyingine kwaajili ya kujifunza isipokuwa Tanzania, tunashukuru sana kwa kuwa majirani wema na kufungua milango kwaajili yetu.” Amesema Mwangi.

Mwangi ameongeza kuwa ataandaa mkataba wa makubaliano (Memorundum of Understanding) kati ya Kenya na Tanzania kutokana na kile ambacho yeye na wennzake wamejifunza ili uwasaidie katika kukuza na kuendeleza uhusiano mwema kati ya Tanzania na Kenya katika sekta ya madini, ambao pia utasaidia kuandaa sera, miongozo, sheria na kanuni ya namna ya kuhakikisha wanatumia rasilimali madini walizonazo kwa manufaa ya nchi yao na wakenya kwa ujumla ikiwemo ukusanyaji wa kodi pamoja na kutengeneza ajira kwa wakenya.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji STAMICO Dkt. Venance Mwasse amefurahishwa na ujio wa ujumbe huo ambao umeona ni vyema kujifunza kutoka Tanzania juu ya shughuli za uchimbaji na usimamizi wa rasilimali madini, huku akiamini kuwa ushirikiano huo utasaidia kukuza diplomasia ya uchumi kati ya nchi hizo.

“Tumejadiliana mengi na tumebadilishana uzoefu wa namna ya kuendesha Sekta ya Madini, nini kinatakiwa kufanyika hasa kwenye maeneo ya masoko, maeneo ya kuendeleza wachimbaji wadogo, lakini kwenye maeneo ya namna Taifa lenye rasilimali hizi linaweza likashiriki kwenye kuzivuna, wameona sisi tumefanya vizuri kwenye maeneo hayo na wamekuja kujifunza, tumewaelezea namna tunavyonufaika na asilimia kumi na sita za hisa za serikali kwenye migodi, tumeeleza pia namna ambavyo Shirika hili la Taifa linanufaika kutokana na hii Sekta ya Madini, lakini pia namna ambavyo tumeweza kurasimisha sekta ndogo ya wachimbaji wadogo ambao wengi ni watanzania.” Amefanunua Mwasse.

Mwasse amesema kuwa watahakikisha wanawatembeza wageni hao katika maeneo mbalimbali ya Shirika hilo ili wajionee namna ambavyo shirika hilo limekuwa likifanya kazi kwa vitendo, huku akisema kuwa wataweka msingi mzuri wa ushirikiano.

“Geolojia haina mipaka, lakini nchi ndiyo zenye mipaka kinachopatikana huku huenda kinapatikana pia kule Kenya, kwahiyo sisi tuko tayari kushirikiana nao kwenda kule kuwasaidia kugundua na kuweza kuona ni namna gani wanaweza wakasimamia rasilimali hizo ili ziweze kunufaisha watu wao.”

STAMICO ni Shirika la madini ambalo linamilikiwa na serikali chini ya Wizara ya Madini, ambapo pamoja na mambo mengine lina majukumu ya kupata makubaliano na kuwa na maslahi katika shughuli yoyote inayohusiana na utafutaji na uchimbaji wa madini, kukuza, kuwezesha au kusaidia mabadiliko ya uchimbaji madini na uchimbaji mdogo kuwa uchimbaji uliopangwa vizuri.

Mwisho

Previous articleBRELA , COSOTA, BPRA, COSOZA WASAINI MAKUBALIANO YA USHIRIKIANO
Next articleSUA YADAHILI WANAFUNZI ZAIDI YA 6000 MAONESHO YA TCU JIJINI DAR
Hughes Dugilo is a Writer, News Producer, Video-Photographer Journalist, and Video Editor experienced for 20 years now performing in News, Documentary, Advertisements and Television Programs. Aside from all above he own and operate his Blog known as Green Waves Media TZ since 2018.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here