Mkalimani wa Lugha za alama akiwasaidia ufahamu watu wenye uhitaji maalum katika mkutano wa Wahariri wakuu wa Vyombo vya Habari ikiwa ni shamra shamra kuelekea maadhimisho ya siku ya kiswahili Duniani ambayo hufanyika kila ifikapo julai 7,hafla iliyofanyika julai 04,2023 katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil Kikwajuni Mjini Unguja.
Na: Rahma Khamisi Maelezo 4/7/2023 .
Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdullah amewataka wahariri wakuu na wanahabari kuchangamkia fursa za kiswahili zilizopo Duniani ili kuendelea kuisambaza lugha hiyo.
Ameyasema hayo katika Ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul-Wakil Kikwajuni katika mkutano wa wahariri wakuu ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani.
Amesema kiswahili ni lugha inayotumika sehemu nyingi duniani hivyo ikitokea fursa yeyote nje ya Tanzania ni vyema kuchangamkia fursa hizo ili kuipaisha zaidi lugha hiyo.
Aidha amefahamisha kuwa wahariri wakuu wana jukumu la kukilinda na kukisambaza kiswahili kwani wao ni watumiaji wakubwa katika shughuli zao mbalimbali wanazozifanya kila siku.
“Wahariri ni wajibu wenu kukitangaza na kukisambaza kiswahili hivyo mtimize majukumu yenu ipasavyo kwani itasaidia kukipeleka mbali ingawa kuna wachache wanaoharibu lugha hiyo,” alifahamisha Makamo.
Amesema kuwa kutokana na hali hiyo ipo haja kwa wahariri kuweka mikakati madhubuti ili kuhifadhi lugha ya kiswahili ,hivyo waendelee kuilinda, kuitunza na kuikuza ili izidi kuenea duniani kote
Makamo ameeleza kuwa Jukwaa la wahariri liwe mfano katika kukitangaza kiswahili na kuwataka kuendelea kuwa na mashirikiano kati yao na Baraza la Kiswahili Zanzibar na Tanzania ili lugha hiyo iendelee kutumika.
“Tukienzi na kukikuza kiswahili kwani ni miongoni mwa tunu ya Taifa letu “alisema Makamu .
Akitoa malezo mafupi kuhisiana na Maadhimisho hayo Katibu Mkuu wa Baraza la Kiswahili Tanzania BAKITA Consolata Pita Mushi amesema maadhimisho hayo yanatokana na maamuzi ya umoja wa Matiafa kua kila ifikapo Julai 7 kuwa ni siku ya Kiswahili duniani ikiwa maadhimisho hayo ni ya pili kufanyika duniani.
Akitoa mada ya Nafasi ya Mhariri Mkuu katika kusimamia matumizi sanifu katika vyombo vya habari Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Charles Hilary amesema wahariri wa vyombo vya habari wana wajibu wa kufanya kazi zao kwa umakini ili kuepusha makosa yasitokee katika matamshi ya kiswahili.
Aidha amesema kuwa baadhi ya vyombo vya habari havifanyi kazi kwa umakini kwani makosa mengi hujitokeza wakati wanapotoa taarifa zao jambo ambalo linaharibu ladha ya lugha hiyo .
Aidha amefahamisha kuwa kuna baadhi ya makosa hutokea wakati wa kuwasilisha taarifa kwani kuna maneno yanatamkwa kinyume na uhalisia ambayo yanasababisha kubadilisha maana ikiwemo ovyo na oye na badala yake hutamkwa hovyo na hoye jambo ambalo lichafua lugha hiyo.
Katika mkutano huo mada mbili zilijadiliwa ikiwemo Nafasi ya wahariri Wakuu katika kukisimamia Kiswahili Sanifu ndani ya Vyombo vya Habari na “uzowefu wa mkuu wa redio china kuonyesha nafasi ya mhariri mkuu katika kusimamia ufasaha na usanifu wa lugha ” ambapo Kauli mbiu ya mwaka huu Kiswahili chetu ni Umoja wetu.