Home BUSINESS DODOMA YAONGOZA KWA WINGI WA MADINI YA AINA TOFAUTI

DODOMA YAONGOZA KWA WINGI WA MADINI YA AINA TOFAUTI

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) leo tarehe 28/07/2023 wamewasilisha taarifa ya utafiti wa Madini yanayopatikana nchini Tanzania huku Dodoma ikiongoza kwa kuwa na orodha ya madini ya aina nyingi.

Akiwasilisha taarifa hiyo leo Meneja Jiolojia kutoka (GST) Bw. Maswi Solomon amesema kuwa utafiti huo umeonyesha miongoni mwa madini matano ya kimkakati madini manne yako katika Mkoa wa Dodoma.

Amesema Mkoa wa Dodoma ni maarufu kwa upatikanaji wa miamba yenye madini ya lithium, chrysoprase, chuma, nikeli, urania na jasi. Aidha, taarifa hiyo imeonyesha kuwa kuna madini ya yoderite yanayopatikana Mlima wa Mautia Wilayani Kongwa na imebainika kuwa madini haya hadi sasa yanapatikana Tanzania pekee duniani kote. 

Akipokea taarifa ya utafiti huo Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amesema taarifa hiyo itakuwa ni nyenzo itakayosaidia  kuutangaza Mkoa wa Dodoma kimkakati husasan katika uwekezaji wa sekta ya madini.

“Nawashukuru sana GST kwa kuwasilisha kitabu hiki na ramani ya inayoonyesha madini katika Mkoa wa Dodoma, ni taarifa muhimu sana ya kuvutia wawekezaji kwa kuwa imeainisha aina ya madini na eneo yanapopatikana” Senyamule amesisitiza.

Aidha, Senyamule pia ametoa wito kwa jamii kutumia taasisi hiyo ya Serikali katika kufanya utafiti wa ardhi kabla ya kuanza kwa ujenzi wa ghorofa katika ya 3-4 ili kuepuka madhara.

Pia, ametoa rai kwa taasisi hiyo kushirikiana na Bonde la Wami Ruvu katika kuendeleza tafifi za wingi wa maji katika bonde hilo kwa kuwa taasisi ya GST imethibitisha kuwa na vifaa na utaalamu wa kutosha.

Jiolojia ya Mkoa wa Dodoma imegawanyika katika makundi manne huku sehemu kubwa ikiwa ni ile ya kundi la miamba ya Archean ya Dodoman na Nyanzian ambayo baadhi yake ni maarufu kwa upatikanaji wa madini ya dhahabu, ila kwa Dodoma miamba hii ina madini ya chuma, urani, nikeli na lithium.

Aina ya pili ni miamba ya Usagaran ambayo ni maarufu kwa uwepo wa madini ya vito, chuma na shaba. Aina ya tatu ya miamba ni ile ya ukanda wa Neoproterozoic Mozambique Mobile Belt inayopatikana Wilaya za Kondoa, Mpwapwa na Kongwa na maarufu kwa madini ya shaba na vito hasa ruby. Aina ya nne ni ile ya Neogene inapatikana katika maeneo ya Farkwa na Mpondi Wilaya ya Chemba, Gonga na Kondoa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here